|
Utoaji huduma ya maji uboreshwe
2006-07-11 09:51:35
Na Mhariri
Hivi sasa tatizo la utoaji wa ankara zisizo sahihi za maji ni kero kubwa mno kwa wananchi wanaopata huduma hiyo hapa nchini. Wananchi wamekuwa wakilalamika kwa muda mrefu kwamba wanapatiwa bili kubwa za maji mara kwa mara.
Kuna wakati wananchi wamelalamika kupokea bili hizo huku wakiwa hawapati huduma hiyo ya maji, au wakiwa wanapata kwa kiasi kidogo sana.
Haifahamiki wahusika wanatumia kigezo gani wakati wakielewa fika kwamba maeneo mengi, hususan ya jiji la Dar es Salaam, yanakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji lakini wao wanaendelea kutoa ankara kubwa.
Ndiyo maana tunaungana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo na Ardhi kwa kuzishauri mamlaka zinazohusika na huduma hiyo kubuni njia sahihi zitakazoondoa kero hii moja kwa moja.
Mjumbe wa Kamati hiyo, Bw. Idd Azzan, ambaye ni Mbunge wa Kinondoni, alisema katika ripoti ya kamati hiyo kwamba huu ni wakati wa mamlaka husika na maji kuingia katika matumizi ya kompyuta katika kuendesha shughuli zao.
Tulitarajia kwamba katika zama hizi za sayansi na teknolojia, mamlaka zinazohusika na maji zingekuwa mstari wa mbele kuboresha utoaji wa huduma zao licha ya tatizo la maji kuendelea kuwepo katika baadhi ya sehemu.
Lakini kutokana na mikakati inayoendelea sasa ya kuboresha huduma za maji katika maeneo mbalimbali nchini, ipo haja kwa mamlaka husika kujiandaa kujikita zaidi katika matumizi ya kompyuta.
Hilo linapaswa kwenda sambamba na kuajiriwa kwa wafanyakazi wenye sifa zinazostahili badala ya mtindo huu wa miaka nenda rudi wa kuamini kwamba mtu yeyote anaweza kufanya kazi katika sekta ya maji.
Kwa hakika hii ni sekta nyeti sana ambayo inahitaji wafanyakazi wenye uwezo kitaaluma.
Kukosekana kwa wafanyakazi wenye taaluma au kuwepo kwa wafanyakazi wasio na sifa zinazostahili kutaendelea kuathiri kwa kiasi kikubwa utoaji wa huduma katika sekta hii nyeti.
Hatutaweza kufanikisha azma ya serikali yetu ya kuhakikisha maisha bora kwa kila Mtanzania kama huduma ya maji itaendelea kutolewa kwa ubabaishaji.
|