09 Jul 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Jamaa akiwa na mahela hashikiki...lakini akiishiwa...
 
2006-07-09 09:47:48
Na Flora Wingia

Fedha zinapatikana kwa njia mbalimbali. Wapo wanaozipata baada ya kufanya biashara fulani, wengine baada ya kazi za maofisini(mishahara) na hata wakulima wanapouza mazao yao. Kwa ujumla ni kipato baada ya shughuli fulani.

Kipato hicho hata hivyo, huingia katika fungu la matumizi. Sasa hapo inategemea mwenye kipato chake amekusudia kukitumia vipi. Wapo wanazitumia pamoja na mambo mengine kusomesha watoto, kuendeleza biashara na miradi mingine ya kuendeleza familia.

Lakini wengine pindi wanapozipata tu, hazitulii mifukoni. Vikao vya marafiki kwenye baa haviishi, kutafutia vimwana wazuri ndiyo usiseme ili mradi tu ionekane mbele za wengine kwamba wanazo za kutosha.Siyo vibaya mtu akatumia mahela yake jinsi apendavyo kwani ni jasho lake.

Pamoja na ukweli huo, wapo wanaojisahau wanatamba sana na fedha tena katika matumizi yasiyo na umuhimu mkubwa na zinapoisha wanajishika tama utadhani walikwapuliwa toka mifukoni mwao. Kumbe walizitoa wenyewe! Hebu sikia kituko hiki.

Nikiwa sehemu hivi majuzi na marafiki zangu tukipata vinywaji, alifika baba mmoja na kutusalimu. Karibu wote tuliokuwa pale alitupatia shikamoo ya nguvu. Wengine ni wadogo zake kiumri lakini alituamkia.

Kisha akamwita kando mmoja wetu na kuteta naye. Kumbe mwenzetu alikuwa anaomba ofa ya kabia kamoja. Jamaa akamwambia akaketi kisha atamtumia bia hiyo.

Ndipo rafiki yetu aliyempa ofa akatusimulia yaliyomsibu baba yule hata kufikia hatua ya kupita meza hadi meza akiomba kinywaji au nauli ya kurejea nyumbani kwake.

Kumbe alikuwa na kazi yake nzuri katika moja ya vyombo vya fedha nchini. Kutokana na fedha kumkubali, aliishi maisha mazuri(kama vijana wa mitaa wanavyoyaita -maisha yaliyoenda shule). Kwenye vikao na marafiki ndio kabisa wakati wote aliwadhihirishia wenzake hakuna anayemfikia kwa mahela.

Kumbe kutamba kote kule, sehemu ya fedha zilikuwa ni za ubadhirifu kwani alisimamishwa kazi, kisha akafukuzwa kabisa.

Hali ile, kulingana na marafiki zake wa karibu, ilimchanganya kiasi cha kushinda katika baa akisaka watu anaowafahamu ili wamsetiri ama kwa fedha au kwa vinywaji.

Ama kwa hakika, hakutegemea kama iko siku moja angepita kuombaomba wakati alitamba sana na fedha huku akidharau wengine kwamba hawamfikii kwa lolote lile.

Isitoshe, hakujua kwamba mpanda ngazi siku zote hushuka, au hata siku moja usinyee kambi kwani waweze kuirejea kisha ukapaona pachungu. Maisha Ndivyo Yalivyo.

Mpenzi msomaji, hizo ndio faida za tambo za fedha. Ipo mifano mingi tu ndani ya familia zetu ambapo mmoja wa viongozi wa familia awe ni baba au mama hubahatika kuwa na kipato kikubwa. Wapo waliotumia vema vipato hivi na wapo waliovichezea na matokeo yake wakayaona muda siyo mrefu.

Wapo baadhi ya kibaba ambao hutamba kwenye vilabu vya pombe na wanapofilisika huenda huko huko vilabuni kujiaibisha(mfano niliyemzungumzia).

Wengine ni kiguu na njia leo na kidosho huyu, kesho yule na kadhalika ili mradi anawabadili kama nguo wavaazo. Wakati huo haelewi kama zitaisha kwani wanachojua zitakuwepo tu siku zote.

Kinamama nao wapo wajanja wajanja wakiwa nazo hudiriki kutoa ofa kwa wachuchu wao kama kazi. Yaani badala ya yeye kusubiri apewe ofa au kuhongwa, yeye ndiye anayefanya kazi hiyo.

Hiyo ni kufuru ya fedha. Nyumbani mtoto akitaka anunuliwe kitu fulani hujibiwa kwa jeuri na wakati mwingine humfukuzilia mbali. Siyo kwamba fedha hazipo, ila zinasubiri kwenda kutoa ofa za bure.

Ngoja mirija zinakotoka fedha hizo izibwe, wengine hata vilabuni hawaonekani wakisingizia wako busy nyumbani kumbe mufilisi.

Kwa wale wasio na aibu utawaona wakirandanda kwenye sehemu za starehe wakisaka marafiki ili wawasetiri. Hawa hawakutambua kwamba kila kitu kina mwisho. Si unajua ule msemo ’ngoma ikilia sana iko karibu kupasuka?’

Watu wajifunze kutokana na makosa ya wengine. Na hakika, ukiona mwenzako kanyolewa, wewe tia maji kabisaaa....Tujifunze kutumia vipato vyetu vizuri na ikiwezekana kujiwekea akiba.

Pia kumbuka fedha zingine hasa zinazopatikana isivyo halali hazina baraka zozote katika matumizi yake. Mtu anabaki kuamini kwamba maadamu zinapatikana basi zitaendelea kupatikana.

Kumbe anajidanganya. Mianya yake ikigundulika ndio hao wanaojikuta kiguu na njia wasijue kwamba wanajidhalilisha wenyewe. Maisha Ndivyo Yalivyo.

Wasalaam

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.