|
Chakula maalum kwa wenye virusi vya ukimwi chafanyiwa utafiti
2006-07-08 09:12:26
Na Raymond Kaminyonge
Taasisi ya Chakula na Lishe nchini(TFNC) inaendelea kukifanyia utafiti chakula maalum kwa ajili ya matumizi ya watu wanaoishi na virusi vya ukimwi huku wakitumia dawa za kurefusha maisha yao na kuongeza kinga katika miili yao.
Mamia ya watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi hapa nchini wamepata fursa ya kutumia dawa zinazowasaidia kurefusha muda wa kuishi maarufu kama ARV\s. Hii ni hatua muhimu katika kuwawezesha watu hao kuendelea kuishi na pia kufarijika.
Hata hivyo, hatua hiyo imeibua tatizo lingine kwa watumiaji wa dawa hizo ambalo ni lishe bora.
Tatizo hili, linatokana na ukweli kwamba dawa hizi zina nguvu kubwa kiasi kinachomlazimisha mtumiaji apate kwanza chakula cha kutosha kabla ya kuzitumia.
Kwa bahati mbaya ni kwamba idadi kubwa ya wagonjwa hawana uwezo wa kumudu kununua vyakula mbali mbali vya kukidhi sharti hilo muhimu kwa watumiaji wa dawa hizo.
Kwa kutambua hilo, Taasisi ya chakula na Lishe, imebuni chakula maalum chenye mchanganyiko wa vyakula vya asili ili kama kitathibitika kukidhi haja, kitumiwe na watu wenye virusi na ambao wanatumia dawa hizo.
Kwa sasa chakula hicho kinafanyiwa utafiti.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Dk.Godwin Ndossi amesema mpango huo ni miongoni mwa mambo mengi yanayofanywa na taasisi yake katika mapambano dhidi ya Ukimwi.
Moja ya majukumu makubwa ambayo Taasisi imekuwa ikiyafanya tangu ilipoanzishwa miaka 33 iliyopita, ni kuielimisha na kuihamasisha jamii ya Kitanzania kuhusu umuhimu wa lishe, anasema Dk Ndossi.
Anasema jukumu hilo ililenga zaidi makundi maalum ya watu katika kijamii.
Makundi hayo ni pamoja na ya wanawake wajawazito, watoto wachanga na watu wenye virusi vya Ukimwi. Taasisi imekwishatengeneza miongozo ya kitaifa kuhusu lishe kwa makundi hayo, anasema.
Anasema kufuatia hatua ya Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuanza kutoa dawa za kurefusha maisha kwa watu wenye virusi, taasisi yake inalazimika kubeba jukumu la kusaidia kutoa ushauri.
Ushauri huo ni wa kuelekeza ulaji bora wa chakula kwa watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi na ambao wanatumia dawa hizi zenye nguvu mwilini, anasema.
Anasema hilo linafanyika sambamba na hatua za kutafiti na kupima ubora wa chakula maalum kilichobuniwa na taasisi ili kitumiwe na wanaotumia dawa za kurefusha maisha.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, chakula hicho kimebuniwa kwa ushirikiano wa wataalam wa taasisi hiyo na wenzao wa Idara ya Uhandisi wa Kemia katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kampuni ya Power Foods.
Uwezo wa chakula hicho utapimwa kwa kuwapa watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi ili wakitumie na watafuatiliwa ili kuangalia kama uzito na kinga inaongezeka mwilini.
Lakini pia kubaini kama maambukizi ya magonjwa nyemelezi ya mara kwa mara yanapungua au lai, anasema.
Utafiti huo utafanywa katika Manispaa za Kinondoni na Temeke.
Anasema kama chakula hicho kitathibitika kuwa kinafaa, basi kitatangazwa ili kuwawezesha wenye tatizo hilo kukitumia.
Utafiti huo alisema umeanza kwa kutoa mafunzo kwa wadau mbalimbali wa masuala ya afya.
Dk. Ndossi anasema pamoja na utafiti huo, taasisi pia itaendelea kutafiti vyakula na mahusiano yake kiafya na kilishe katika makundi yaliyo katika hatari ndani ya jamii .
Lakini pia kubuni michanganyiko yenye kiwango cha juu cha ubora ili kukidhi mahitaji ya wenye VVU/Ukimwi, anasema.
Kamishina wa Tume ya Kudhibiti Ukumwi Nchini (TACAIDS), Askofu Sylivester Gamanywa anasema chakula kina nafasi ya pekee katika suala zima la huduma na tiba kwa wanaoishi na VVU na wenye Ukimwi.
Anasema pamoja na kwamba suala hilo liko wazi, lakini lishe na Ukimwi ni mambo ambayo hayajapewa msukumo wa kutosha katika jamii.
Nchi yetu ina vyakula ambavyo vina virutubisho muhimu vinavyohitajika katika kuboresha lishe kwa wanaoishi na ugonjwa huo.
Tatizo kubwa ni kuwa jamii haijaelimishwa au kuhamasishwa vya kutosha kuhusu kuandaa na kuchanganya vyakula ili viweze kukidhi mahitaji yanayokusudiwa, anasema Askofu Gamanywa .
Kamishna huyo anasema vyakula kutoka nje ya nchi ni vya ghali ikilinganishwa na uwezo wa watu wengi.
Hii ina maana kuwa vyakula hivyo ni vya wenye uwezo tu, pale ambapo vyakula vyetu sisi wenyewe vinaweza kuchanganywa na kutoa bidhaa ambazo kila mtu anaweza kuizpata kwa gharama nafuu ni vizuri hilo likafanyika na kwa kweli itakuwa ni faida kubwa kwa jamii yetu anasema.
Anatoa changamoto kwa taasisi hiyo na wadau wengine kuendelea na ubunifu wa michanganyiko mbalimbali ili kupata bidhaa nyingi bora na salama kwa matumizi ya kilishe.
Mwenyekiti wa SHDEPHA+, Bw. Joseph Kato aliwahi kusema kuwa kuwapa dawa watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi bila kuangalia uwezo wao wa kupata lishe bora ni sawa sawa na bure.
Anasema dawa ya kuongeza muda wa kuishi haiwezi kumsaidia mtu anayeishi na virusi vya Ukimwi bila pia kumsaidia kupata lishe.
Anasema dawa hizo zina nguvu kubwa.
|