07 Jul 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Manispaa ya Kinondoni na kero ya taka
 
2006-07-07 10:07:37
Na Grace Chilongola

Jiji la Dar es Salaam kwa miaka mingi linakabiliwa na tatizo la kushindwa kuzoa takataka zinazozalishwa na kusababisha mlundikano wa takataka katika maeneo mengi.Hivi karibuni timu ya uboreshaji kanda ya Dar es Salaam iliendesha semina kwa madiwani wa manispaa ya Kinondoni juu ya wajibu na majukumu ya viongozi wa kisiasa katika huduma ya usafishaji. Grace Chilongola wa Shirika la Habari la PST anaeleza zaidi kuhusu huduma ya usafishaji kwenye manispaa hiyo.

Mwanaisha Juma (si jina halisi) anagongewa mlango asubuhi wakati akitayarisha kifungua kinywa na mara anasikia kelele iliyokuwa inatoka kwa kijana mmoja ... ’’tunazoa taka lete mia saba kabisa taka nyingi kweli kweli’’.

Anapofungua mlango anakutana na kijana huyo,anayesukuma mkokoteni uliojaa taka. Bi. Mwanaisha anabisha kidogo na kumweleza anazo sh. mia tano tu.Lakini kijana yule anabisha akitaka aongezewe ujira.,’’ Hizo ndiyo pesa nilizonazo kama unatakabeba la sivyo ziache tu kwa kuwa bado ni kidogo.

BiMwanaisha ni kati ya maelfu ya wakazi wa wilaya ya Kinondoni wanaotegemea wabeba taka binafsi badala ya huduma hiyo ya kubeba takataka kushindwa kutolewa na Halmshauri ya Manispaa hiyo pamoja na wakala walioteuliwa na mamlaka hiyo.

Kutokana na hali hiyo ukipita katika mitaa ya manispaa ya Kinondoni kila baada ya hatua kadhaa utakutana na mlundikano wa taka ambao bado hazijazolewa na kwenda kutupwa kwenye dampo.
Malundo haya ya takataka katika maeneo mbalimbali ndani ya manispaa hiyo husababisha harufu mbaya inayokera kwa wapita njia na baadhi ya maeneo ya makazi ya watu.

Manispaa ya Kinondoni yenye ukubwa wa eneo la ekari 3030 ina wakazi 1,088,867 wanaozalishwa tani zaidi ya 1,064 za takataka kwa siku.

Licha ya wingi wa wakazi hao manispaa hiyo inapanuka kwa haraka mno na kutokana na ujenzi wa kasi, imekuwa ni vigumu kupata eneo la dampo la kutupia taka.

Zaidi ya asilimia 70 ya wakazi wa manispaa ya Kinondoni wanaishi katika makazi yaliyojengwa kiholela na kusababisha msongamano unaosababisha baadhi ya maeneo kutofikika kwa urahisi kwa magari jambo linaloathiri pia uzoaji taka Kulingana na taarifa kutoka ofisi hiyo.

Meya wa manispaa ya Kinondoni Bw. Salum Londa anasema ingawa manispaa hiyo inazalisha taka nyingi kiasi hicho inao uwezo mdogo wa kuziondoa ambapo wakandarasi uwezo wao ni kuzoa kati ya asilimia 27 na 30 ya taka zinazozalishwa.

Kiasi hicho ni kidogo mno na juhudi za makusudi zinahitajika kuzoa taka hizo kufikia angalau asilimia 60 yaani tani 638 ya taka zote zinazozalishwa kwa siku.

Bw. Londa anaeleza ili kuweza kufikia lengo la kuzoa asilimia 60 yaani tani 638 za taka zinazozalishwa kwa siku moja, halmashauri ya manispaa ya Kinondoni inahitaji zaidi ya Sh. milioni 200 kwa mwezi.

Licha ya gharama kubwa ya kuzoa taka kwa mwezi yapo matatizo mengi yanayoikimba shughuli hiyo ikiwani pamoja na uwezo mdogo wa wakandarasi wanaotoa huduma na usimamizi hafifu wa halmashauri katika ngazi ya kata na mtaa.

Pia makandarasi licha ya kukabiliwa na tatizo la upungufu wa magari na vifaa,wanalo pia ugeni katika kazi hiyo na pia ushiriki hafifu wa wadau wakubwa ambao ni jamii inayozalisha taka hizo.

Katika uchunguzi wake, PST iligundua, baadhi ya familia za kipato cha chini hushindwa kuwalipa wazoa taka binafsi na hivyo hutumia mbinu za kuweka taka hizo kwenye viroba na kuzitelekeza katika maeneo ya uficho au kwenye magofu ya nyumba.

”Chakula chenyewe cha tabu hiyo hela ya kumplipa mzoa taka nitatoa wapi ” Ramla mkazi wa Mwananyamala ambaye anasema biashara yake kubwa ni kuuza maandazi.

Kutokana na uwezo mdogo wa wakandarasi wanaozoa taka, mara nyingi vituo vya kupokea taka hufurika kwa sababu ya kutokuwepo kwa gari la kusomba taka. Vivyo hivyo makazi mengi huwa na mrundikano wa taka nyingi zenye kutoa harufu mbaya kwa sababu ya kukaa muda mrefu bila kuzolewa licha ya wakandarasi hao kuingia mkataba ya kuzoa taka na wakazi hao.

Mstahiki Londa anakiri,’’Hali ya usafi katika manispaa hairidhishi, maeneo mengi ya makazi bado yamejaa taka ambazo hazizolewi na nyingine zinatupwa kwenye mabonde, mabwawa na mito inayozunguka maeneo ya makazi’’.

Manispaa na viongozi wake wakiwepo wenyeviti wa mitaa na madiwani hawana utaratibu wa kufuatilia uzoaji huu holela wa taka ili kujua wanaozizoa hupeleka kuzitupa dampo lipi.

Uchunguzi uliofanywa na PST katika mitaa ya manispaa hiyo,umegundua kwamba wazoaji taka wanaotumia mikokoteni, baadaye huzibwaga popote na hasa kando ya viwanja vya michezo, shule au kwenye madaraja, mito na mabonde.

Kutoka na ongezeko la haraka la watu na ukuaji wa makazi ya watu manispaa ya Kinondoni lipo tatizo la eneo la kuanzisha dampo la kutupa takakata na sasa taka zinaposombwa hutupwa eneo la Mtongoni ,Temeke ambapo si dampo rasmi.

Uelewa mdogo na kipato duni cha wakazi juu ya umuhimu wa uwekaji mazingira yanayowazunguka katika hali ya usafi na yenye kupendeza imekuwa ni chanzo cha matatizo ya uchafuzi wa mazingira.

Kwa upande wa uendeshaji, uwezo mdogo wa kukabiliana na ongezeko kubwa la taka kutokana na kuwa na vitendea kazi duni na bajeti finyu inaypotengwa kwa ajili ya utoaji huduma ya usafishaji imekuwa ni tatizo pia.Pamoja na jitihada zinazofanywa za uzoaji taka na uafishaji kwa ujumla bado manispaa katika siku za hivi karibuni inaweza kupatwa na tatizo kubwa la ukosefu wa mahali pa kutupia taka.

Pia dampo kuwa katika makazi ya watu ambapo yamekuwa yakisababisha kero kubwa, harufu mbaya na kuhatarisha maisha ya wakazi wanaolizuguka kwa kusababisha magonjwa ya mlipuko.

Katika kushiriki kupitia na kupitisha mipango mbalimbali ya halmashauri, Diwani ana nafasi nzuri ya kupendekeza njia za kuboresha uwezo wa watendaji wa halmashauri hasa katika eneo la udhibiti wa taka.

Mshauri miundo na rasilimali watu, katika mpango wa uboreshaji serikali za mitaa, Bw. Geofrey Luvimbi, anasema suala la taaluma bora katika udhibiti wa taka ni muhimu likapewa kipaumbele ili kuwawezesha watendaji kuwa na mipango mipya, bora na yenye ufanisi, kadri changamoto la kero ya udhibiti wa taka linavyoongezeka katika miji yetu.

Diwani kama kiongozi anapewa hadhi ya uongozi kutokana na hamu ya jamii inayompa hadhi kutaka kuona anafanya kazi ya kuleta mabadiliko mazuri na endelevu kwa jamii.

Akizungumzia wajibu na majukumu ya viongozi wa kisiasa hususan katika huduma ya usafishaji anasema halmashauri ni mwezeshaji wa utekelezaji katika suala zima la udhibiti wa taka. Suala la usafishaji linahitaji ushiriki kamilifu wa wadau wote.

Ni muhimu kuweka mazingira muafaka ili suala la udhibiti wa taka lizungumziwe kwa lugha moja katika ngazi ya jamii yenye mtazamo ulio muafaka wa malengo, mikakati na ukubali wa uwajibikaji wa pamoja na wanajamii katika ngazi mbalimbali utawezesha kuiweka manispaa nafasi nzuri ya uzoaji wa taka.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.