|
Tanzania yatoa milioni 56 kwa ajili ya ujenzi wa Bwawa la kuhifadhia maji
2006-07-16 19:00:36
Na EAR Habari
Serikali nchini Tanzania imetoa shilingi milioni 56, kwa ajili ya ujenzi wa Bwawa la kuhifadhia maji ili kuimarisha kilimo cha umwagiliaji, katika kata ya Misozwe wilayani Muheza mkoani Tanga.
Ujenzi wa bwawa hilo unasimamiwa na ofisi ya umwagiliaji kanda ya Kilimanjaro iliyopo chini ya wizara ya kilimo na chakula, kwa lengo la kuendeleza kilimo cha umwagiliaji, kukuza tija katika uzalishaji mazao ya chakula na biashara, kuongeza mapato ya wakulima wadogo na kuondoa umaskini.
Mhandisi wa kilimo cha umwagiliaji kanda ya kaskazini Bw. Kulwa Saimon, amesema hayo katika ufunguzi wa mafunzo ya uhamasishaji wakulima skimu ya umwagiliaji maji mashambani iliyofanyika katika kijiji cha Misozwe wilayani Muheza.
|