|
Mwili wa mwanaume Dar waokotwa mtoni
2008-05-17 15:14:42
Na Mwanaidi Swedi, Jijini
Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Shaaban Abdallah, 30, amekutwa amefariki dunia kwenye mto wa maji ya Chai Jijini.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Temeke, Emmanuel Kandihabi, amesema tukio hilo limetokea jana, majira ya saa 3:00 usiku katika eneo la Mbagala Mbande.
Kamanda Kandihabi amesema Polisi walipata taarifa toka kwa baba mzazi wa kijana huyo, Bw. Abdallah Said, 49, ambaye ameeleza kuwa siku hiyo alimkuta mtoto wake kwenye mto huo akiwa amefariki.
Amesema marehemu alioneka sehemu ya miguu ndani ya karavati la mto huo na sehemu nyingine ya mwili haikuwa ikionekana.
Aidha, amedai kuwa kijana huyo alitoweka nyumbani tangu tarehe saba mwezi huu na kuonekana jana akiwa tayari amefariki.
Kamanda Kandihabi amesema chanzo cha kifo hicho bado hakijafahamika na kwamba hadi sasa, mwili wake umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Temeke.
Wakati huohuo, mwanaume mmoja ambaye jina lake halikuweza kuhafahamika mara moja, na anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 25 na 30, amefariki dunia kwa kupigwa na wananchi wenye hasira.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Temeke, Emmanuel Kandihabi, amesema tukio hilo limetokea jana, majira katika eneo la Yombo Kilakala.
Kamanda Kandihabi amesema mwanaume huyo aliuawa kutokana na tuhuma za wizi, lakini haikufahamika ni wapi alifanya wizi huo.
Amesema mwili wa marehemu huyo umehidadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali ya Temeke.
|