|
Vijana 200 wa Kisarawe waula
2008-05-16 16:13:25
Na Claudia Kayombo, Kisarawe
Wanafunzi zaidi ya 200 wa shule mbalimbali katika Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe wameula baada ya kunufaika na msaada wa zaidi ya Sh. Milioni 53 zilizotolewa na asasi moja ya kimataifa ya Plan International.
Wanafunzi hao wamesomeshwa katika kipindi cha kati ya mwaka 2006 na mwaka huu.
Kaimu Meneja wa asasi hiyo ya kimataifa ya Plan International, Bw. Suleiman Jaffu, amesema vijana walionufaika na msaada huo ni wale wanaoishi katika mazingira magumu na wenye wazazi wasiojiweza kiuchumi.
Bw. Jafu amesema katika kipindi cha mwaka 2006 shirika hilo liliwapeleka vijana 50, katika vyuo mbalimbali vya ufundi hapa nchini ili kuwakomboa na tatizo la ukosefu wa ajira.
Meneja huyo akafafanua katika kipindi hicho shirika lilitumia Sh. 5,449,850 kugharamia ada ya masomo hayo ya ufundi.
``Katika kipindi cha mwaka juzi tuliwapeleka vijana 50 katika vyuo mbambali hapa nchini ambapo shirika lilitumia kiasi cha Sh. 5,449,850 kugharimia ada za masomo hayo,`` akasema Bw. Jafu.
Akaongeza katika kipindi cha mwaka 2007 vijana 80 walipelekwa vyuoni na shirika liliwagharamia ada ya Sh. Milioni 24.
Kwa upande wa mwaka huu, akasema vijana 80, pia wamepelekwa vyuoni kwa gharama ya Sh. Milioni 24.
Akasema mafunzo wanayokwenda kujifunza vijana hao ni pamoja na uuguzi, ushonaji, umakanika, ufundi umeme.
Meneja huyo, akafafanua katika kipindi cha mwaka juzi, shirika lilitenga bajeti ya kutosha kwa ajili wa vijana wengi zaidi ya hao lakini waliojitokeza ni vijana 50 tu idadi ambayo ilikuwa chini ya bajeti waliyopanga.
Hata hivyo, akasema kuwa mwaka jana na mwaka huu idadi kubwa ya vijana walijitokeza na kutaka msaada huo lakini bajeti yao iliwezesha kuwagharamia vijana 80 tu.
Kuhusu idadi ya vijana waliopata ajira baada ya kumaliza mafunzo hayo, Bw. Jafu akasema shirika limepanga kufanya tathmini ya vijana wanaowasomesha na sehemu wanazofanyia kazi.
Hata hivyo, akasema wengi wa vijana waliopata mafunzo ya mwaka mmoja katika kipindi cha mwaka juzi, wameajiriwa katika sehemu mbalimbali hapa nchini.
|