|
Wananchi Boko walia na matukio ya wizi, ujambazi
2008-05-16 16:07:05
Na Mwandishi Wetu, Jijini
Wakazi wa Boko nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, wameomba Jeshi la Polisi kuwadhibiti wamiliki wa bar na wenye vituo vinavyoonyesha picha za video mitaani nyakati za usiku na kwenye vilabu vya pombe vinavyoendesha shughuli zake usiku kucha.
Aidha, wamelalamikia kitendo cha baadhi ya magari ya doria ya Polisi kuegeshwa bar muda mrefu, wakidai kuwa askari husika wa doria wanaweza kupata vishawishi kirahisi toka kwa wahalifu na hivyo kuweza kushirikiana nao katika matendo yao ya wizi na ujambazi.
Wakizungumza katika kikao cha pamoja baada ya matukio zaidi ya 10 mfululizo, wamesema vilabu vya pombe za kienyeji, bar na maeneo ya kuonyeshea video na sinema za usiku vinaweza kuwa sehemu ya maficho ya wezi na majambazi wanaosumbua eneo hilo.
Wakasema kuwa kilabu kimoja maarufu cha kuuza pombe katika eneo hilo kinaendeha shughuli zake usiku kucha na kuwa kero kwa wananchi waishio eneo hilo, huku pia kukiwa na hofu kuwa mahala hapo panaweza kuwa maficho ya wahalifu.
Wajumbe waliwataja baadhi ya maofisa ambao wamekuwa wakikalia taarifa za uhalifu kutoka kwa raia wema na wengine kuzigeuza mradi kuwa ni wa kutoka katika vituo vya Ununio, Bunju na Wazo.
Pia wajumbe hao wamebaini vijiwe viwili ambavyo hutumiwa na wahalifu hao ambavyo ni vya eneo la Mtambani na kingine kilichopo nje ya saluni moja iliyo jirani na duka la mfanyabiashara mmoja maarufu wa eneo hilo.
Aidha, wakazi hao wamewasilisha majina 10 ya watu wanaotuhumiwa kuhusiana na matukio ya wizi na ujambazi katika eneo hilo kwa kamishana wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Alfred Tibaigana.
Akizungumza na gazeti hili amesema kuwa atamuagiza Kamanda wa Wilaya husika kulishughulikia tatizo hilo na kwamba muda si mrefu, tatizo hilo litakomeshwa.
|