|
Wadau wa mazingira waumiza vichwa kuhusu changamoto ya taka ngumu
2008-05-16 16:06:22
Na Mwanaidi Swedi, Jijini
Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira, NEMC, Bi. Anna Machungwa, amesema tatizo la kuzagaa kwa taka ngumu bado ni changamoto kubwa kwao na wadau wengine wa mazingira nchini.
Bi. Machungwa ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani, inayoadhimishwa Juni 5 ya kila mwaka.
Amesema kwa mwaka, nchi zaidi ya 180 duniani zinatarajiwa kuadhimisha siku hiyo ambayo kwa mwaka huu kauli mbiu yake ni Badili Mazoea, Jenga Uchumi Endelevu kwa kudhibiti Uzalishaji wa Gesi Joto.
Hata hivyo Bi. Machungwa amesema ujumbe wa kitaifa wa siku hiyo ya mazingira ni Hifadhi Mazingira, Dhibiti Uchomaji Moto, Panda Miti.
Akizungumzia suala nzima la kudhibiti taka ngumu, Bi. Machungwa amesema kisheria suala hilo linashughulikiwa na mamlaka za Serikali za mitaa na manispaa katika maeneo husika.
Akasema mamlaka hizo ndizo zenye jukumu la kuchukua hatua pale taka hizo zinapojitokeza katika maeneo yake na kuwa ugumu wa udhibiti wa tatizo hilo unajitokeza pale baadhi ya wahusika wanaposhindwa kutekeleza wajibu wao wa kusimamia.
Amesema Baraza la NEMC ni mdau muhimu katika suala nzima la kusimamia utupaji taka kwa kuhakikisha maeneo yanayoandaliwa yanakamilika kwa kuzingatia taratibu ziliwekwa kisheria.
Bi. Mchungwa akasema baraza hilo linao wajibu wa kuhakikisha linasimamia mazingira kisheria na kufanya usafi katika maeneo ambayo wahusika wameshindwa kuyafanyia usafi kisha wahusika wazembe kulipishwa gharama zinazohitajika.
Pia amezungumzia tatizo la uchafuzi wa mazingira unasababishwa na magari ambapo amesema NEMC inafanyamazungumzo na SUMATRA ili kuwataka wahakikishe vyombo vyao vya usafiri vinavyochangia uharibifu wa mazingira zinachukuliwa hatua kama si kuondolewa.
Amesema baraza hilo linaweza kumchukulia hatua mtu yeyote kwa mujibu wa sheria pindi anaposhindwa kutekeleza kanuni za usafi kwenye maeneo yanayomzunguka.
|