|
Majambazi Dar yatembeza mapanga, yapora mapesa
2008-05-16 16:03:26
Na Moshi Lusonzo, Jijini
Mwanaume mmoja mkazi wa Kimara Baruti, amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akiwa taaban baada ya majambazi kuvamia nyumba yake na kuanza kumpiga ili awape pesa.
Mtu huyo ametambulika kwa jina la Joseph Charles, 42 na kwa sasa anapatiwa matibabu katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili, MOI, kufuatia majambazi hayo kumjeruhi vibaya kwa kumpiga kwa mapanga eneo la kichwani.
Kwa mujibu wa Afisa Uhusiano wa MOI, Bw. Almas Jumaa, mtu huyo amefikishwa kwao majira ya saa 8:00 usiku.
Akasema ndugu waliomfikisha hapo wameeleza kuwa majambazi hayo, mara baada ya kumvamia, yalianza kumpiga kabla ya kumpora kiasi cha pesa kisichofahamika hadi sasa.
Walioshuhudia tukio hilo, wamesema majambazi hayo yalimvamia Bw. Charles na familia yake wakati wakijiandaa kulala.
Wakasema majambazi yalipongia ndani kwa Charles, yakawa yakitaka Charles kuonyesha mahali anakotunza pesa zake.
Wakasimulia kuwa wakati wakiwa katika hali ya majibizano, ndipo majambazi hayo yalipoanza kumkatakata kwa mapanga kichwani na kumfanya apoteze fahamu zake.
Alipofikishwa hapo, haraka alikimbizwa chumba cha upasuaji na kushonwa sehemu zilizoathirika kichwani mwake kabla ya kupatiwa kitanda wodini ili aendelee na matibabu zaidi.
|