|
Viongozi wa mitaa Kinondoni wapewa mbinu kudhibiti VVU
2008-05-15 19:52:43
Na Grace Chilongola, PST-K`ndoni
Viongozi wa mitaa mbalimbali ya Manispaa ya Kinondoni wameanza kupata mafunzo juu ya mbinu mbalimbali za kudhibiti ongezeko la maambukizi ya ukimwi katika maeneo yao.
Akifungua mafunzo hayo ya siku tatu ya wajumbe wa Kamati za Kudhibiti ukimwi katika mitaa ya manispaa hiyo, Bw. Joseph Sonya ambaye ni Diwani wa Kata ya Mwananyamala amesema viongozi hao ni muhimu katika mapambano yanayoendelea dhidi ya ukimwi.
Akasema hiyo inatokana na ukweli kuwa wao wako karibu zaidi na wananchi, hivyo inakuwa rahisi kwao kupata takwimu sahihi juu ya maambukizi ya virusi vya ukimwi, VVU.
Iwapo kila mshiriki atazingatia mafunzo haya ya kujengewa uwezo kwenye sehemu zenu za kazi, ni wazi kwamba atapata elimu ya kupambana na maambukizi ya gonjwa hili yeye binafsi na jamii inayomzunguka, akasema Diwani Chonya.
Akawataka washiriki hao kutekeleza kwa vitendo yale yote wanayojifunza katika semina hiyo.
Awali, Mratibu wa Ukimwi katika Manispaa ya Kinondoni, Bi. Mercy Ndekeno, alisema mafunzo hayo yanalenga kuziwezesha kamati za ukimwi kutekeleza majukumu yao katika mapambano dhidi ya ukimwi.
Bi. Mercy akasema baada ya kupatiwa mafunzo hayo, Manispaa inatarajia kupata takwimu sahihi za ukimwi kutokana na ukweli kuwa zilizopo sasa zimebainika kuwa zina mapungufu kadhaa.
Akitoa mada ya wajibu na majukumu ya kamati za kudhibiti ukimwi, Bi. Mercy akawataka washiriki hao kushirikiana na asasi zisizo za kiserikali zinazojishughulisha na mapambano dhidi ya ukimwi katika kupata takwimu sahihi za watu wanaoishi na virusi vya ukimwi ili mipango ya kuwasidia ifanyike kwa usahihi.
Mafunzo hayo ndani ya Manispaa ya Kinondoni yanafanyika kwa kuhusisha wajumbe wa mitaa 62 kati ya 127 iliyopo katika mwaka huu wa fedha wa 2007/08.
|