|
TASAF yamwaga mamilioni kukamilisha miradi Kinondoni
2008-05-15 19:50:53
Na Francisca Jeremiah, Kinondoni
Awamu ya pili ya utekelezaji wa kazi za Mfuko wa Mendeleo ya Jamii nchini, TASAF, umetumia Sh.1,230,784,330.00 kwa kuendeleza miradi mbalimbali katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kwa kipindi cha mwaka 2007 hadi Machi 2008.
Hayo yamesemwa na Meya wa Manispaa ya Kinondoni Bw. Salum Londa, wakati alipokuwa akizungumza na Alasiri kuhusiana na manufaa waliyoyapata kutokana na uwepo wa mfuko huo.
Amesema mfuko huo umeleta maendeleo makubwa kwani ulifadhili miradi mingi kwa asilimia 101, ingawa awali ilipanga kutumia Sh.1,223,051,520.00 na badala yake ilitumia Sh.1,230,784,330.00.
``Mfuko huo umetusaidia sana... miradi mingi ya jamii iliyotekelezwa imesaidiwa na TASAF. Kama mfuko huo usingekuwepo, nadhani hali ingekuwa vigumu zaidi kwetu,`` akasema Bw. Londa.
Meya Londa akaitaja baadhi ya miradi iliyofadhiliwa na TASAF kuwa ni pamoja na ya ujenzi wa zahanati sita, vyumba 14 vya madarasa ya shule za sekondari, vivuko vinne vya waenda kwa miguu 4, ujenzi wa visima vya maji vitano, miferji ya mvua 13, vyumba vinne vya vya madarasa katika shule za msingi na vyoo viwili na nyumba mbili za walimu.
Hata hivyo, akasema Halmashauri hiyo inahitaji Sh. Bilion Saba kwa ajili ya ujenzi wa shule za sekondari za kata tisa ili waweze kuchukua wanafunzi wanaomaliza shule ya msingi kwa asilimia 95.
Akasema katika chaguo la kwanza, walishindwa kuchukua wanafunzi wengi kutokana na ukosefu wa vyumba vya madarasa ambapo waliofanikiwa kujiunga ni 7,376 kati ya waliofauli15,937, sawa na asilimia 46.3.
Bw. Londa alisema mwaka huu Manispaa imejitahidi kuandikisha watoto wengi wa shule ya msingi wapatao 23,599 sawa na asilimia 95.6, wakiwa na matumaini kuwa watakapomaliza wataweza kuendelea na masomo ya sekondari kutokana na ujenzi wa shule hizo unaoendelea kila kukicha.
|