13 May 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Mafisadi: Majina yatua ikulu
 
2008-05-13 17:54:43
Na Mwandishi wetu, Jijini

Hatimaye ile orodha ya watumishi wa Serikali wanaotuhumiwa kushiriki dili lililoiwezesha kampuni ya kuzalisha umeme ya Richmond kuweza kuingia mkataba wa kifisadi ulioiingiza nchi katika hasara ya mabilioni ya pesa imetua ikulu kwa ajili ya kusubiri hatua za kiutawala kuchukuliwa dhidi yao.

Akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari, Waziri Mkuu Bw. Mizengo Pinda amesema tayari Katibu Mkuu Kiongozi Bw. Philemon Luhanjo ameshakabidhiwa orodha ya wahusika na na kupewa maelekezo ya kuchukua hatua za kiutawala.

Amesema Bw. Luhanjo anatakiwa kuchunguza na kuwachukulia hatua watumishi wote wa Serikali wanaotuhumiwa na sakata hilo la mkataba `bomu` wa Richmond, lililozua gumzo kubwa nchini.

Akasema Katibu Mkuu Kingozi ataanza kwa kuwachukulia hatua watuhumiwa wote waliotajwa kwenye ripoti ya Kamati Teule ya Bunge, iliyochunguza mkataba wa Richmond.

Miongoni mwa watuhumiwa waliohusishwa na sakata hilo na kutakiwa kujiuzulu kutokana na kuzembea ama vinginevyo, kutokana na ripoti ya Kamati hiyo ya Bunge ni pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw. Johnson Mwanyika, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, TAKUKURU, Bw. Edward Hosea na Mkurugenzi wa Nishati na Madini katika Wizara ya Nishati na Madini Bw. Bashir Mlindoko.

Kwa mujibu wa mapendekezo ya kamati hiyo teule ya Bunge iliyokuwa chini ya Mwenyekiti wake Dk. Harrison Mwakyembe, kigogo mwingine anayepaswa kuchukuliwa hatua za kinidhamu ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Bw. Arthur Mwakapugi.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Pinda, watuhumiwa hao wanaweza kutimuliwa kazini au kupunguziwa madaraka, kutokana na uzito wa makosa yao au vinginevyo, kadiri sheria zitakavyoruhusu.

``Maelekezo yote amepewa Katibu Mkuu, suala hili sasa linafikia mwisho kwa kuwa anaandaa hatua za kuwachukulia, kama ni kuwafukuza kazi au kuwateremsha vyeo, well and good,`` akasema Bw. Pinda.

Waziri Mkuu amesema hivi sasa Serikali haikubali kuchafuliwa na hivyo kila anayebainika kujihusisha na vitendo vya rushwa na ufisadi anawajibishwa.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.