|
Majambazi Dar yavamia gesti tena
2008-05-13 17:53:45
Na Mwanaidi Swedi, Temeke
Matukio ya nyumba za kulala wageni almaarufu kama gesti kuvamiwa na majambazi usiku na kisha watu kuporwa mali zao yameendelea kutokea Jijini ambapo baada ya kuripotiwa kule Gongolamboto Mwisho wa Lami, sasa tukio kama hilo limejiri tena Mbagala Jijini.
Kwa mujibu wa taarifa za kipolisi, kundi la majambazi zaidi ya kumi limevamia gesti moja na kufanikiwa kupora vitu mbalimbali venye thamani ya zaidi ya shilingi milioni tatu.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Temeke, Emmanuel Kandihabi, amesema tukio hilo limetokea jana majira ya saa 9:00 usiku katika eneo la Mbagala.
Kamanda Kandihabi amesema majambazi hao wamevamia nyumba ya kulala wageni iliyofahamika kwa jina la Evasti Zakiem, ambayo ina vyumba 12.
Amesema miongoni mwa majambazi hayo, mmoja alikuwa na bunduki aina ya short gun na akarusha risasi kadhaa hewani kwa lengo la kuwatawanya wananchi na kuiba vitu mbalimbali vyenye thamani ya shilingi milion 3,613,000.
Kamanda Kandihabi amesema kabla ya wizi huo kufanyika, alifika mteja mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Athuman Hamisi na kukodi chumba namba 12.
Amesema pia alimuomba mhudumu wa vyumba hiyo Bw. Chacha,19, kumfungulia muda huo kwani anataka kusafiri.
Amesema kuwa ilipofika muda wa saa 9:00 usiku, baada ya mhudumu kumfungulia na ndipo majambazi wale walipoingia na kufanikisha jaribio lao la uporaji.
Hata hivyo, amesema mteja yule aliyejitambulisha kwa jina la Hamisi hakukamatwa, kwani aliondoka mara tu baada ya majambazi kutowekea kusikojulikana.
Kamanda Kandihabi amesema kuwa hadi sasa, Polisi wanaendelea na uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo.
|