|
Pemba hofu tupu!
2008-05-13 17:51:41
Na Sharon Sauwa, Mikocheni
Wananchi wa visiwa vya Pemba, Zanzibar wametawaliwa na hali ya hofu kutokana na kile walichodai kuwa wenzao wanane waliotiwa mbaroni kwa tuhuma za uhaini kutojulikana walikopelekwa.
Watu hao walidakwa baada ya kudaiwa kuwa waliandika barua Umoja wa Mataifa kutaka Pemba ipewe ruksa ya kujitenga.
Akiongea na Alasiri, Mbunge wa Wawi (CUF), Bw. Hamad Rashid Mohamed amesema mpaka hivi sasa wananchi ambao ndugu zao walidakwa wamekuwa na wasiwasi mkubwa kwa hisia kuwa huenda jamaa zao wakawa sehemu isiyo na usalama.
Amesema ukamataji wa watu hao haukuzingatia sheria kwa sababu hakukuwa na mashahidi wala karatasi ya kukaguliwa wakati walipokamatwa.
``Kuna mzee mmoja anayejulikana kwa jina la Hamed Manshedi alipokwenda kukamatwa, ndugu zake walijaribu kusogelea karibu, lakini wakafukuzwa eneo hilo,`` amesema Bw. Rashid.
Amesema kitu kingine kinachotia wasiwasi ni polisi kushindwa kuwaeleza ni wapi watuhumiwa hao wanakoshikiliwa.
Amesema tayari jambo hilo zito wamelifikisha kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bw. Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda na Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Said Mwema.
``Nikiwa Pemba jana nilituma ujumbe kwa viongozi hao lakini mpaka sasa sijapata majibu,\"amesema mbunge huyo ambaye pia ni kiongozi wa kambi ya upinzani Bungeni.
Amesema katika barua hiyo inayolalamikiwa, wananchi kadhaa wa Pemba waliandika barua na kupeleka ofisini za Umoja wa Mataifa wakilalamikia masuala kadhaa ya kisiasa kisiwahi humo ikiwa ni pamoja na suala la muafaka.
``Hayo mambo ya Pemba kujitenda hayakuwemo. Mambo waliyokuwa yakilalamikiwa ni ya msingi na sioni sababu ya watu hao kukamatwa na Polisi,`` akasema.
Naye Naibu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa CUF,
Bw. Salum Bimani amesema hofu imetanda katika visiwa hivyo kwa kuwa mambo ya watu kudakwa na kupelekwa kusikojulikana si mageni kufanyika.
Amesema katika kipindi cha kati ya mwaka 1964 na 1972, kuna watu walikamatwa na Polisi mpaka leo hawajulikani wako wapi na kama bado wako hai.
|