|
Mwenyekiti wa CCM Dar awatetea wasiolipia ada
2008-05-13 17:49:29
Na Valery Kiyungu, Makurumla
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Dar es Salaam, Bw. John Guninita, amewataka viongozi wa ngazi zote wa CCM Jijini kutowafukuza kundini wanachama wao wanaoshindwa kulipia ada za kadi zao za uanachama kwa wakati.
Badala yake, Mwenyekiti huyo amewaagiza viongozi hao wa CCCM kuendelea kuwatambua kuwa ni wanachama wao halali.
Bw. Guninita ameyasema hayo wakati alipokuwa akizungumza na wanachama wa chama chake wa Kata ya Makurumla, wilaya ya Kinondoni wakati akizungumza nao kwenye ukumbi wa Shule ya Msingi Mianzini.
``Nadhani si vizuri kutimua wanachama... hata wanaposhindwa kulipa ada kwa wakati, wapeni muda wa kufanya hivyo,`` akasema Bw. Guninita.
Akasema kuwa hatua hiyo inalenga katika kuhakikisha kuwa CCM na jumuia zake inaendelea kuwa na wanachama wake, hasa katika kipindi hiki ambapo CCM inajiandaa katika chaguzi zake zijazo za viongozi.
Bw. Guninita amesema kuwa si vyema viongozi kufukuza wanachama kwa sababu ambazo zinaweza kurekebishwa, hivyo amewataka wahusika kuendesha zoezi la kudai ada kwa wanachama kwa umakini ili wasije kupoteza wanachama walio nao.
Amesema kuwa ni vyema viongozi wakabuni utaratibu wa kutembelea wanachama nyumba hadi nyumba na kuzungumza nao juu ya kulipa ada ya kadi, sambamba na kumpa muda zaidi wa kulipa, kwa yule ambaye atakuwa tayari kuweka ahadi ya kulipa.
Katiaka ziara yake hiyo, Bw.Guninita alifuatana na Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Kinondoni Bw. Aron Mwaikambo na viongozi wengine wa CCM na jumuiya zake.
Aidha, kiasi cha Sh. 518, 200 zimepatikana katika mchango wa wanachama wa kata hiyo ya Makurumla wa papo kwa papo, huku Bw. Guninita akiwa amechangia Sh. 100,000, kwa ajili ya shughuli za kuimarisha chama katika kata hiyo.
|