|
Mahita: Soo lake laibuliwa tena upya
2008-05-12 18:44:18
Na Mwandishi Wetu, Jijini
Baada ya kuwa kimya kwa kitambo sasa, hatimaye lile soo la kudaiwa kutelekeza mtoto linalomkabili aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Bwana Omar Mahita limeibuliwa upya tena.
Kwa mtaji huo, soo hilo litaanza kuunguruma kortini kesho.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo Alasiri imezipata toka katika mahakama ya wilaya Kinondoni ambako shauri hilo la madai limepelekwa, ni kwamba litaanza kusikilizwa baada ya pande zote mbili kukubali kuwa lisikilizwe na Hakimu wa Mahakama ya Wilaya.
Awali, kesi hiyo ilikuwa kwa Hakimu Mkazi Kisutu kabla ya kufutwa mbele ya Hakimu Pellagia Khadaye aliyemtaka mdai kufungua kesi yake kwa Hakimu wa Wilaya.
Kabla ya hapo, wakili wa mdaiwa Mahita, Bw. Charles Semigalawe, aliwasilisha madai ya kupinga kesi hiyo kusiklilizwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi ambapo baada ya kuahirishwa mara kadhaa, hatimaye makubaliano ya pande zote yalifikiwa na sasa kesi hiyo itaanza kuunguruma kwa Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni kesho, kuanzia saa 2:00 asubuhi.
Katika kesi hiyo, mdai ni Bi. Rehema Shaaban, anayeeleza kuwa wakati alipokuwa mtumishi wa ndani wa Bw. Mahita, alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na bosi wake huyo (Mahita) na hatimaye akapata ujauzito.
Anadai kuwa baada ya hapo, Bw. Mahita alimtaka arejee kwao Kondoa na kwamba atakuwa akimpa matunzo.
Ilidaiwa zaidi kuwa baada ya kuwa kwao, mdaiwa Mahita alikiuka makubaliano yao na hivyo Rehema na mwanae wa kiume wakakosa matunzo.
Kutokana na kutelekezwa huko, Bi. Rehema anaiomba mahakama imuamuru Bw. Mahita amtambue mtoto aliyemtelekeza kuwa ni wake na pia, alipe fidia kadhaa ikiwa ni pamoja na kulipia matunzo ya mtoto toka alipomzaa hadi pale mahakama itakapotoa hukumu ya shauri hilo.
|