|
CUF&CCM sasa ni vurugu!
2008-05-12 18:43:10
Na Sharon Sauwa, Mikocheni
Kauli ya Chama cha Mapinduzi, CCM, kwamba CUF wamewadanganya Watazania kuhusiana na muafaka, imezidi kuleta vurugu tupu, kwani wana ngangari nao wamejiandaa kujibu mapigo.
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, ameliambia gazeti hili kuwa, chama chake kinajiandaa kujibu kauli hiyo ya CCM.
Amesema baada ya kauli hiyo, kimepanga kuitisha mkutano wa waandishi wa habari fasta fasta ili kumwaga ukweli wote hadharani.
Amesema katika mkutano huo, uliopangwa kufanyika kesho, CUF watajibu tuhuma zinazotolewa na CCM kuhusiana na suala la muafaka.
Jana, katika mkutano wake, CCM walidai kuwa wanasikitishwa na upotoshaji wa makusudi unaofanywa na viongozi wakuu wa CUF kuhusiana na mwenendo wa mazungumzo ya muafaka.
Katibu Mkuu wa CCM, Bw. Yusuf Makamba alisema pia CUF wamekiuka makubaliano ya msingi kuhusu kutangaza maamuzi yanayofikiwa na vyama hivyo katika mazungumzo.
Akasema walikubalina kwamba katika kutoa taarifa ya maamuzi yaliyofikiwa ni lazima kutolewa kwa pamoja na makatibu wakuu wa vyama hivyo (Makamba na Hamad pichani ukurasa wa mbele ).
Alisema pia walikubaliana mwenendo wa mazungumzo uwe na usiri na itakapolazimika kutoa taarifa kwa wananchi, basi wawepo makatibu wakuu.
Kuhusu upotoshaji Mwenyekiti Mwenza wa Timu ya CCM katika muuafaka, Mzee Kingunge Ngombale Mwiru alisema CUF walikwenda kutangaza kwamba muundo wa serikali shirikishi Zanzibar una nafasi ya Waziri Kiongozi ambaye atatoka chama kilichopata ushindi wa pili.
Akasema ukweli ni kwamba mapendekezo ya timu hiyo yanafuta nafasi ya Waziri Kiongozi na kuweka nafasi mbili za Makamu wa Rais.
|