|
Mwanaume Dar adaiwa kujiua baada ya `bifu` na mkewe
2008-05-12 18:42:08
Na Kiyao Hoza, Polisi Kati
Mwanaume mmoja aliye mkazi wa Jijini anadaiwa kujitoa uhai wake kwa kunywa dawa ya kuulia wadudu wa pamba baada ya kutokea mtafaruku baina yake na mkewe.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Faustine Shilogile, amesema tukio hilo limetokea jana mishale ya saa 5:00 asubuhi pale Gongo la Mboto Mikongeni.
Amemtaja mwanaume huyo kuwa ni Sebastian Eliyo, 33, anayedaiwa kunywa sumu aina ya Thiodan aliyokuwa ameichanganya katika dawa ya kuchanganyia rangi ya Tina.
Kamanda Shilogile amesema mwanaume huyo anadaiwa kufikia uamuzi huo baada ya kugombana na mkewe, hata hivyo chanzo cha ugomvi huo hakijajulikana.
Amesema mtu huyo alifariki pale pale na mati yake imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Amana na uchunguzi zaidi unaendelea.
|