|
Bosi wa taasisi ya mikopo Dar aibiwa gari kanisani
2008-05-12 18:39:29
Na Usu-Emma Sindila, Jijini
Watu wasiofahamika na wanaosadikika kuwa ni majambazi wamepora gari la Afisa mikopo wa Pride kwa kutumia funguo bandia wakati mwenyewe akiwa ameliegesha nje ya kanisa kwa ajili ya ibada ya sala ya jana Jumapili.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Jamal Rwambow amesema tukio hilo limetokea jana mishale ya saa 7:00 mchana huko Ubungo Makuburi, nje ya Kanisa Katoliki Parokia ya Makuburi.
Amesema mwenye gari hiyo Bi. Chrisensia Saktai, 39, akiwa na watoto wake wawili waliingia katika kanisa hilo mishale ya saa 5:00 asubuhi kwa nia ya kwenda kusali.
Ameongeza kuwa baada ya kumaliza kusali, Bi. Chricensia alipotoka nje ya kanisa na kwenda kuangalia alikopaki gari lake yenye namba za usajili T 720 AUG aina ya Toyota Corolla, hakulikuta na hivyo kuamua kutoa taarifa polisi.
Kamanda Rwambow amesema msako zaidi wa kutafuta gari hilo unaendelea na hakuna mtu yeyote aliyekamatwa hadi sasa kuhusiana na tukio hilo.
Wakati huohuo, Opereta wa mashine ya kufyatua matofali na mkazi wa Boko Jijini, Said Kitila, 23, amefariki dunia baada ya kupigwa na shoti ya umeme wakati akiwa kazini.
Kamanda Rwambow amesema tukio hilo limetokea jana mishale ya saa 7:00 mchana huko Boko Basihaya.
Amesema wakati kijana huyo akiwa anaendelea na shughuli za kufyatua matofali, mashine aliyokuwa akiitumia ilipata hitilafu ya umeme na kumnasa.
Ameongeza kuwa wakati marehemu akihaika kujitoa katika mashine hiyo, mfanyakazi mwenzake ambaye ni mchanga mchanga aliyetambulika kwa jina moja la Alex, 28, alikwenda kuzima soketi ya mashine hiyo ndipo Said alipodondoka chini na kuwahishwa katika hospitali ya karibu lakini ikagundulika tayari alishafariki dunia.
Kamanda Rwambow amesema maiti imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Mwananyamala kwa uchunguzi zaidi.
|