12 May 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Wakulima wa mboga Bagamoyo waomba kuchimbiwa mabwawa
 
2008-05-12 18:37:11
Na Sabina Mgellah, PST - Bagamoyo

Wakulima wilayani hapa wameiomba serikali kuwasaidia kusaka wafadhili wa kuwachimbia mabwawa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.

Wakiongea na PST, wakulima hao wa Chalinze na Vigwaza wamedai kuwa, pamoja na kuwa Serikali inahimiza kilimo cha umwagiliaji, bado kilimo hicho kinakwamishwa na ukosefu wa mabwawa makubwa.

Wakulima hao wamedai kuwa hivi sasa, kilimo chao cha mboga mboga na matunda kinategemea zaidi maji ya mabonde, ya mito na mabwawa machache yaliyopo.

``Kwa hapa Chalinze, tuna vikundi vya ushirika ambavyo vinafanya shughuli zake kwa ushirikiano na tumeshachanga pesa mara kadhaa kwa ajili ya uchimbaji wa mabwawa lakini bado maji hayatoshi kwa kilimo,`` akadai mkulima mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Bi. Mwahija Ramadhan.

Aidha, wamesema kuwa katika kipindi hiki cha mvua nyingi, kilimo chao kinakwenda vizuri kutokana na kuwepo kwa maji ya kutosha lakini ugumu wa shughuli hizo wanaupata hasa kipindi cha kiangazi ambapo hakuna mvua.

Walisema endapo watasaidiwa kuchangiwa kiasi fulani cha fedha na serikali ama na wafadhili kwa ajili ya kuchimbia mabwawa hayo, wanauhakika wa kuhifadhi maji ya kutosha hata baada ya mvua kuacha kunyesha.

Naye Mkuu wa Wilaya hiyo Luteni Kanali Mstaafu Serenge Mrengo, amewapongeza wakulima hao kwa jitihada zao za kuendeleza kilimo cha umwagiliaji.

Hata hivyo, Mkuu huyo amewataka wakulima hao kutovunjika moyo kwa kukosa wafadhili na amewaahidi kushirikiana nao katika kutafuta wahisani hao ili waweze kupata mabwawa ya kutosha.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.