12 May 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Vijana Bagamoyo watakiwa kuacha kushinda vijiweni
 
2008-05-12 18:35:10
Na Sabina Mgellah, PST - Bagamoyo

Halmashauri ya wilaya ya Bagamoyo imewataka vijana kutafuta mbinu halali za kujipatia kipato badala ya kushinda vijiweni wakicheza bao huku wakiilaumu Serikali kuwa haiwajali.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bi. Rhoda Nsemwa wakati akihojiwa na PST kuhusiana na malalamiko ya vijana wilayani hapa ya kutowekewa kipaumbele katika kupatiwa misaada.

Mkurugenzi huyo amesema kila kijana ana wajibu wa kujituma kufanya kazi pamoja na kubuni mbinu mbadala za kujipatia kipato badala ya kujibweteka na kuingojea Serikali katika kila jambo.

``Sasa kama wewe kijana mwenye viungo vyote kamili unaacha kujishughulisha na kuishia kuilaumu Serikali kila kukicha, wazee na wenye ulemavu nao wasemeje? Ni lazima wabadilike sasa ili wajiletee maendeleo,`` akasema Bi. Rhoda.

Aidha, amewataka vijana wasiokuwa na ajira kubuni biashara zinazoweza kuwapatia vipato na sio kujibanza vijiweni na kuishia kuwapora wapita njia mali zao.

Amesema, ingawa Serikali inafanya kila jitihada katika kuwasaidia vijana kwa kuwapatia mikopo midogo midogo, bado kuna kila sababu kwa vijana hao kuacha kuingojea Serikali ambayo kamwe haitaweza kumsaidia kila mtu kwa wakati wake.

Pia ameongeza kuwa wilaya ya Bagamoyo bado ina vijana wengi ambao wanazurula mitaani na kupiga debe katika vituo vya mabasi pasi na kazi nyingine maalum, sababu kubwa ikiwa ni kutokana na ukweli kuwa baadhi yao huacha shule mapema na wengine kurubuniwa na wenzao na kujiingiza katika makundi yasiyofaa.

``Vijana wajiunge kwenye vikundi vya uzalishaji... hakuna njia ya mkato ya kujikwamua kiuchumi zaidi ya kujituma katika kazi. Kushinda vijiweni hakuwezi kuwaondoa na janga la umaskini,`` akasema Bi. Rhoda.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.