|
Yanga wapigana `Vijembe`
2008-05-12 18:33:57
By Jacqueline Massano, Jijini
Mweka hazina wa Yanga, Abeid Abeid `Falcon` amepinga kauli iliyotolewa na katibu mipango, Patrick Fatta ya kuwaita baadhi ya wanachama kuwa ni `makomandoo` na kudai si ya kiungwana kwani inaweza ikaleta mtafaruku klabuni.
Mwishoni mwa wiki, Fatta amekaririwa na gazeti moja (siyo Alasiri), akidai makomandoo wanaojichomeka ndani ya klabu ndiyo chanzo kikubwa cha kudidimiza maendeleo.
Fatta amedai baadhi ya viongozi wa Yanga wanaogopa kwenda makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo katika makutano ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam, kutokana na kuwakwepa makomandoo hao.
Bosi huyo amedai wameshindwa kuwaondoa kirahisi kwa kuwa wao ni wanachama halali na waliosajiliwa.
Akizungumza na Alasiri mapema leo, Abeid amewapongeza wanachama hao kwa sababu ni wachapakazi wa klabu na wala si makomandoo kama katibu huyo anavyodai.
``Si kweli na si haki kuwaita wanachama makomandoo, kwa kuwa hayo makundi yalivunjwa muda mrefu wakati wa muafaka, sasa unapoleta suala la makomandoo kwenye klabu ni kuvuruga amani ndani ya klabu.`` amesema.
Abeid amesema kama suala la matumizi na mapato yeye (Fatta) akiwa kama katibu mipango wa klabu hakupaswa kuyaelezea kwa sababu hayamuhusu na ni kazi ya mweka hazina.
Bosi huyo amesema kinachotakiwa kufanya ni kuhakikisha amani inakuwepo ndani ya klabu ikiwa ni pamoja na kufanya usajili wa maana kwa msimu ujao na wala si kuwazungumzia makomandoo.
|