|
Jamhuri Kihwelo apewa Simba
2008-05-12 18:33:06
By Badru Kimwaga, Jijini
Hatimaye uongozi wa klabu soka ya Simba umeamua kumrejeshea ulaji, kocha Jamhuri Kihwelo `Julio` kuongoza jahazi la timu hiyo baada ya kupoteza matumaini ya kumrejesha aliyekuwa kocha mkuu, Mserbia Milovan Cirkovic, aliyedaiwa kuikacha timu kutokana na kumaliza mkataba wake wa awali.
Cirkovic, aliingia mkataba wa miezi mitatu kuifundisha Simba huku akilipwa mshahara na kundi la `Friends of Simba`, ambao baadaye ikadaiwa wamejiondoa katika jukumu hilo.
Habari za kuaminika toka ndani ya Simba na kuthibitishwa na mmoja wa viongozi wa klabu hiyo zinasema, Julio amekabidhiwa timu huku akitafutiwa msaidizi wake ili waweze kuiongoza timu katika michuano ya Kombe la Kagame itakayofanyika nchini mapema Julai.
``Uongozi umetafakari kwa makini na kuamua kumrejeshea katika ukocha mkuu, Julio kutokana na kukaa na kuzoeana na wachezaji kwa muda mrefu, na ndiye atakayesajili wachezaji na kuiongoza timu katika michuano ya Kombe la Kagame,`` amesema kiongozi huyo.
Kiongozi huyo amesema tumaini la Milovan kurejea katika timu hiyo ni dogo kutokana na ukweli klabu kwa sasa haina fedha.
Amesema walikubaliana na kocha huyo kwenda kupumzika kwao kwa miezi miwili, lakini kutokana na kujitoa kwa walipaji wa mshahara wake, itakuwa ngumu kumrejesha tena kocha huyo nchini.
Ameongeza ingawa Julio hajafahamishwa rasmi kutokana na ukweli kwa sasa ana jukumu zito katika kikosi cha timu ya mkoa wa Ilala `Tsere Boys`, lakini atafahamishwa mara muda muafaka utakapofikiwa na hasa baada ya kamati ya utendaji kukutana na kujadili suala la usajili mpya wa Simba.
Kabla ya kushushwa cheo na kuwa kocha msaidizi, Julio ndiye aliyekuwa kocha mkuu wa muda akirithi mikoba ya Twalib Hillal aliyechukuliwa kuziba nafasi ya Mbrazil Nielsen Elias aliyeifundisha Simba kwa muda wa siku 39 tu na kulala mbele kutokana na ubabaishaji wa viongozi wa timu hiyo.
|