10 May 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Karamagi, mambo magumu
 
2008-05-10 19:41:42
Na Sharon Sauwa, Mikocheni

Lile soo la mkataba wa kampuni ya Kimataifa ya Upakuaji wa Makontena Bandarini (TICTS), lililosababisha aliyekuwa Waziri wa Nishati Bwana Nazir Karamagi, kuwekwa kitimoto Bungeni limechukua sura mpya ambayo inazidi kumweka pabaya mwanasiasa huyo.

Wakati Karamagi bado anasubiri hatma ya vielelezo vyake alivyowasilisha kwa Spika, kuhusiana na madai aliyoyatoa bungeni wakati anaitetea TICTS juu ya utendaji wake, wanasiasa kadhaa wameibana kampuni hiyo na kuitaka icheue tenda ya kutoa huduma za upakuaji mizigo bandarini iwapo kazi hiyo imeishinda.

Karamagi ni mmoja wa wamiliki wa kampuni hiyo alifichua ukweli huo katika kikao cha bunge kilichopita wakati kampuni hiyo ilipokuwa ikilalamikiwa kwa kile kilichodaiwa kuwa utendaji wake ni doro.

Akiongea na Alasiri Mbunge wa Mbozi Kusini (CCM), Godfyey Zambi, amesema madai yanayotolewa na kampuni hiyo kwamba imeshindwa kufanya kazi kwa ufanisi kutokana na ukosefu wa eneo la kutosha, ni visingizio tu.

Mbunge huyo ambaye ndiye aliyewasilisha hoja binafsi bungeni akilalamikia utendaji wa TICTS, anasema kampuni hiyo ilipaswa kuwa na mpango wa biashara kabla ya kuomba kutoa huduma katika bandari hiyo.

``Haya walipaswa kuyajua mapema, hawa walipewa eneo Ubungo muda mrefu wakasuasua sana kuanza kulitumia...hivi ni visingizio tu,`` akasema Bw. Zambi.

Kauli hiyo inafuatia maelezo yaliyotolewa na kampuni hiyo kwa vyombo vya habari majuzi, ambapo pamoja na mambo mengine ilijitetea kuwa inakabiliwa na ufinyu wa eneo la kuhifadhia makontena wanayopakua kwenye meli kutokana na wafanyabiashara wanaoyaagiza kutoyaondoa kwa wakati.

Mbunge huyo aliendelea kudai kuwa kampuni hiyo inatumia vifaa ilivyokabidhiwa tangu wakati ilipopewa nafasi ya kutoa huduma katika bandari hiyo badala ya kuongeza vyake.

Akafafanua kuwa asilimia 66 ya vifaa vinavyotumika katika bandari hiyo ni vichakavu.

Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amesema suala la mkataba linatakiwa kuwa la uwazi na linalofuata utaratibu na hivyo kuweza kuweka ushindani katika tenda ya utoaji wa huduma.

Amesema suala la TICTS linaathiri kwa kiasi kikubwa uchumi wa nchi kwa kuwa bandari ni raslimali inayotegemewa si tu na Watanzania bali pia na nchi jirani zisizo na bandari.

``Wao walipokabidhiwa kutoa huduma katika eneo hilo, kwanini hawakuibua jambo hilo wanalolizungumza hivi sasa kwa wakati huo na kusubiri hadi karibu muda wa mkataba kwisha?... nadhani kuna tatizo,`` akasema Profesa Lipumba ambaye pia ni mtaalamu wa masuala ya uchumi.

Kwa upande wake, Mbunge wa Karatu (CHADEMA), Dk. Wilbroad Slaa, amesema kampuni hiyo ilipaswa kulijua mapema tatizo la ufinyu wa eneo kabla ya kuanza kuomba nafasi ya kutoa huduma.

Amesema uamuzi wa mkutano wa 11 wa Bunge, uliotolewa baada ya Bw. Zambi kuwasilisha hoja yake binafsi juu ya utendaji usioridhisha wa kampuni ya TICTS, unabaki pale pale na kwamba haitakiwi kuyumba.

Katika hoja yake, Bw. Zambi alitaka Serikali isitishe nyongeza ya mkataba wa miaka 15 kwa kampuni hiyo na kufanya mapitio ya mkataba wa awali ili vifungu vya mkataba huo ambavyo havina manufaa kwa taifa virekebishwe.

Pia aliitaka Serikali baada ya muda wa mkataba wa awali wa miaka 10 ambao unamalizika mwaka 2010, nyongeza mpya izingatie sheria namba 21 ya mwaka 2004 inayotoa fursa kwa makampuni kushindania tenda katika utoaji huduma.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.