|
Banda la biashara Manzese lawaka moto
2008-05-10 19:39:52
Na Kiyao Hoza, Polisi Kati
Wanafunzi wawili wamejeruhiwa vibaya baada ya kibanda walichokuwamo ndani yake kuteketea kwa moto Jijini Dar.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Jamal Rwambow, amesema tukio hilo limetokea jana mishale ya saa 4:30 asubuhi pale katika eneo la Manzese Midizini.
Amesema moto huo uliteketeza kibanda cha biashara cha Bw. Ally Ndoka, 40, na kuteketeza mali yote iliyokuwamo ndani yake inayokadiriwa kuwa na thamani ya Sh.400,000.
Kamanda Rwambow amesema chanzo cha moto huo ni mshumaa na dawa ya mbu iliyokuwa imewasha na wanafunzi hao aliowataja kuwa ni Hamisi Masasi, 18, mwanafunzi wa kidato cha kwanza, Tegeta Sekondari na mwenzie Abeid Ally mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Ukombozi.
Amesema vijana hao wamejeruhiwa sehemu mbalimbali mwilini na wamelazwa katika Hospitali ya Mwananyamala.
Amesema moto huo ulizimwa na wananchi wa eneo hilo.
Wakati huohuo, mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Tandika, Wema Chigomo, 15, amezimia na kulazwa katika hospitali ya Temeke baada ya kutokea vurugu wakati wa mchezo wa mpira wa miguu wa kirafiki baina ya Sekondari ya Tandika na Mbagala.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Emmanuel Kandihabi, amesema tukio hilo limetokea jana mishale ya saa 8:00 mchana katika Uwanja wa mpira wa Tandika Mabatini.
Kamanda Kandihabi amesema katika mchezo huo Mbagala ilifungwa bao 2-0, na ndipo ilipoanzisha fujo ikiwamo kutupiana mawe.
Amesema kutokana na fujo hizo wanafunzi hao kila mmoja alianza kukimbia kivyake na ndipo mwanafunzi huyo alipozimia na kukimbiziwa katika hospitali ya Temeke.
Kamanda Kandihabi amesema hadi polisi inapata taarifa hizo, mwanafunzi huyo alikuwa bado akitibiwa hospitalini hapo.
|