|
Waziri Mkuchika apigia debe lugha za Kiafrika
2008-05-10 19:36:52
Na Haji Mbaruku, Jijini
Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Bw.George Mkuchika amezitaka nchi za kiafrika kufanya mapinduzi ya kifikra na kiutamaduni ili kutoa nafasi ya kukuza lugha za kiafrika.
Waziri Mkuchika amesema wakati akizungumza katika kituo kimoja cha redio Jijini kuwa, sasa wakati umefika kwa waafrika kubadilika kuhusu lugha.
Alikuwa akiongea na kituo kimoja cha Redio Jijini.
Waziri Mkuchika amesema hayo kufuatia kuendelea kuwepo kwa kasumba kuwa lugha ya kiingereza ndiyo inayotamba kwenye soko la sasa la utandawazi.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa endapo waafrika wenyewe wataamua kuwa na mikakati thabiti, lugha za kiafrika zitapewa kipaumbele.
Hivi karibuni, shirika moja lisilo la kiserikali la Acalan lilifanya kongamano hapa Jijini kuhusiana na lugha za kiafrika.
Katika kongamano hilo, mijadala mbalimbali kuhusu lugha za kiafrika ilijadiliwa.
Waziri Mkuchika alikaririwa akisema kwenye kongamano hilo kuwa, watahakikisha lugha za kiafrika zinakuzwa na kupata nafasi.
Ameitaka jamii iondoke na mawazo hasi kuwa lugha za kiafrika hazifai kufundishia shuleni na vyuoni.
|