|
Wafanyakazi wa boti iendayo kasi wanaswa na `heroine`
2008-05-10 19:35:56
Na Sharon Sauwa, Mikocheni
Wafanyakazi wawili wa boti ziendazo kasi Zanzibar za Sea Bus II, wametiwa mbaroni kwa tuhuma za kupatikana na gramu 30 za madawa ya kulevya ya aina ya heroin.
Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia Madawa ya Kulevya Nchini, Godrey Nzowa, ameiambia Alasiri kuwa watu hao wamekamatwa jana saa 9:00 jioni katika bandari ya Dar es Salaam.
Akawataja watu hao kuwa ni Daud Bakari ambaye ni mhudumu na mdogo wake Hassan Bakari ambaye ni kibarua wa kuuza vinywaji.
Akielezea tukio hilo, Kamishna Nzowa akasema watuhumiwa hao waliweka madawa hayo katika bahasha na kisha juu yake kuweka fedha kaisi cha shilingi 10,000.
Akasema Hassan alipohojiwa na Polisi wakati huo kuwa amebeba nini na alikuwa akipeleka kwa nani, akasema kuwa amebeba pesa na anampelekea kaka yake aitwaye Daudi.
Akasema alipoitwa, Daud akakiri kuwa Hassan ni mdogo wake na kwamba alikuwa akimletea pesa.
Hata hivyo, alipoulizwa pesa pekee amebeba? Alijibu kuwa ndio, kisha akatimua mbio.
Kamishna Nzowa akasema walimkimbiza na kumkamata na kisha kumhoji ni kwa nini alitaka kukimbia wakati anasema kuwa mzigo alioletewa ni pesa.
Akasema kwakuwa madawa hayo ni aina ya `brown heroin`, alipopewa kibano zaidi akasema ni dawa ya kienyeji na alikuwa akimpelekea mgonjwa.
Wakati huohuo, mkazi wa Magomeni Mapipa aitwaye Hemed, amekamatwa na kete 11 za madawa ya kulevya aina ya heroin na kete tatu za bangi.
Akasema hivi sasa, kutokana na kupanda kwa bei ya madawa hayo, wauzaji wamekuwa wakichanganya kete moja ya heroin na kete moja ya banghi.
Akasema watuhumiwa hao wanashikiliwa na Polisi kwa mahojiano zaidi kabla ya kufikishwa mahakamani.
|