|
Henry awachefua Simba
2008-05-10 19:33:33
By Mwandishi Wetu, Jijini
Kiungo Henry Joseph amezidi kuuchefua uongozi wa klabu yake ya Simba, kutokana na kuonyesha utovu wa nidhamu zaidi kwa kukacha kikao cha kamati ya utendaji kilichokuwa kimeitishwa juzi kumjadili.
Habari toka ndani ya klabu hiyo na kuthibitshwa na mmoja wa viongozi wa Simba zinasema kuwa pamoja na kiungo huyo kupewa taarifa juu ya kikao hicho hakuweza kutokea kujitetea, hivyo kuahirishwa.
Kikao hicho kilishindwa kufanyika kutokana na baadhi ya wajumbe wake wakiwemo viongozi wakuu Mwenyekiti Hassani Dalali na Makamu wake, Omar Gumbo kutoonekana kikaoni.
Katibu Mwenezi wa Simba, Seydou Rubeya, amekiri kushindwa kutokea kwa mchezaji huyo ambaye pia ni nahodha wa timu ya taifa, Taifa Stars licha ya kwamba alijulishwa juu ya kuwepo kwenye kikao ili kusikiliza utetezi wake.
Seydou amesema hawajui ni kitu gani ambacho kilimfanya mchezaji huyo asije kwenye kikao hicho wakati alishaambiwa kingefanyika Mei 8 kabla ya kuahirishwa kwa sababu zilizoshindwa kuzuilika.
Hata hivyo, amesema bado wana subiri utetezi wa kiungo huyo mara kikao chao kitakapoitishwa tena baadaye mwezi huu, ili kumjadili na kutoa hatma yake pamoja na masuala mengine ya klabu hiyo.
Kiungo huyo alisimamishwa na uongozi wa Simba kwa tuhuma za utovu wa nidhamu baada ya kushindwa kusafiri na timu kwenda Kagera kucheza mechi ya Ligi Kuu kati yao na Kagera Sugar bila ya kutoa taarifa zozote.
Hata hivyo, uongozi wa Simba ukadai Henry alikacha mechi hiyo kwa ajili ya kufanya hujuma ili timu yao ifungwe na Yanga katika mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu huku ikielezwa na mapenzi na wana Jangwani hao.
Mara aliposimamishwa na kutakiwa kujitetea Mei 8, klabu ya Yanga ilitangaza kutaka kumsajili kiungo huyo kwa madai ya kuonyesha mapenzi na timu yao, ingawa mwenyewe amekuwa akikanusha kutaka kujiunga Yanga.
|