09 May 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Balali hana ujanja!
 
2008-05-09 19:21:02
Na Emmanuel Lengwa, Jijini

Licha ya Serikali kutoa taarifa inayodai kuwa hivi sasa haimtafuti aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu Dokta Daudi Balali ambaye inasemekana amejichimbia Marekani, baadhi ya wanasiasa nchini wanasema, msomi huyo hana ujanja na kinachotakiwa ni kumrejeshwa nchini fasta fasta ili aeleze ni vipi mabilioni ya Watanzania yalichotwa na kuliwa hivihivi.

Imeelezwa kuwa kinachotakiwa kufanyika ni uchunguzi kuendelea kufanywa huku mtuhumiwa akiwa tayari ametiwa mikononi mwa dola kama inavyofanyika kwa watuhumiwa wengine wa makosa mbalimbali.

Akizungumza na Alasiri leo asubuhi, Katibu Mkuu wa chama cha upinzani cha,CHADEMA, Dk. Wilbrod Slaa, amesema sheria ya Tanzania kuhusu makosa ya jinai iko wazi na kamwe haichagui mtu na wala haiangalii hali yake kuwa ni tajiri au maskini.

Akasema kwa mujibu wa sheria za nchi, mtuhumiwa wa makosa ya jinai anapaswa kukamatwa, kufunguliwa jalada polisi na kisha uchunguzi wake kufanywa wakati mtuhumiwa akiwa nyumbani kwa dhamana au rumande.

Dk. Slaa amesema sheria inasema kesi ambayo hairuhusu mtu kukamatwa au kufungwa ni ya madai pekee.

\"Tuhuma zinazomkabili Dk. Balali ni za wizi wa mabilioni ya fedha... hilo ni kosa la jinai.

Sasa kwanini asitafutwe na kukamatwa? Sasa wanaposema wanachunguza, watafanya hivyo kwa RB ipi?\" akahoji Dk. Slaa.

Amesema kinachotakiwa kwa mujibu wa sheria ni kuwakamata watuhumiwa wote wa ufisadi, kuwafungulia RB polisi na kisha uchunguzi kufanyika wakati watuhumiwa wakiwa rumande au wakiwa nje kwa dhamana.

Jana Waziri wa Fedha na Uchumi Bw. Mustafa Mkulo alikaririwa na vyombo vya habari akidai kuwa aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu Bw. Balali ametoweka na hajulikani alipo.

Hata hivyo, taarifa zilizotolewa jana kwa waandishi wa habari na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu Bw. Salva Rweyemamu, zimedai kuwa hivi sasa, Serikali haina shida na Dk. Balali na kwamba itamtafuta wakati utakapowadia baada ya uchunguzi wa sakata lake kukamilika.

Dk. Balali alipigwa chini na Rais wa Jamhurio ya Muungano wa Tanzania Bw. Jakaya Kikwete baada ya ripoti ya mkaguzi wa hesabu za BOT, kampuni ya ukaguzi ya kimataifa ya Ernst & Young, kubaini kuwa kuna mapesa mengi yametumika visivyo wakati akiiongoza taasisi hiyo.

Kashfa kubwa iliyotikisa nchi na kumfanya Balali apigwe chini na Rais ni ile ya kuchotwa kwa zaidi ya Sh. Bilioni 133 za BOT, ambazo zililipwa isivyo halali kupitia akaunti ya malipo ya madeni ya nje, EPA.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.