|
Wanafunzi tisa wa sekondari Dar mbaroni
2008-05-09 19:20:24
Na Kiyao Hoza, Polisi Kati
Wanafunzi tisa wa kidato cha tano na sita katika shule ya sekondari ya Green Acres ya Jijini Dar es Salaam wamefanya fujo kubwa iliyosababisha uharibifu wa magari matatu likiwemo difenda la Polisi.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Jamal Rwambow amesema wanafunzi hao walianza fujo hizo shuleni hapo jana mishale ya saa 7:00 mchana.
Amesema baada ya Polisi kupata taarifa waliamua kukimbilia huko kutuliza ghasia hizo, lakini walipofika eneo la tukio na wao wakaanza kushambuliwa na wanafunzi hao.
Ameyataja magari yaliyoharibiwa wakati wa fujo hizo kuwa ni namba za usajili T 270 ALL aina ya Toyota Prado, T 755 AAQ aina ya Toyota Surf na PT O986 aina ya Land Rover Deffender, mali ya Jeshi la Polisi.
Kamanda Rwambow amesema chanzo cha fujo hizo ni wanafunzi wa shule hiyo wa kidato cha tano na sita ambao hawamtaki Mkuu wa shule hiyo na mwalimu wa nidhamu.
Amesema wanafunzi hao tisa wa kidato cha sita wanashikiliwa na Polisi kuhusiana na fujo hizo.
Kamanda Rwambow akawataja wanafunzi hao kuwqa ni Ramadhan Rashid, 20, Aldin Mataba, 16, Gerard Mahaji, 20, Fred Francis, 20, Mtima Malatu, 18, Haji Mohamed, 19, Samwel Kapamba, 20, Michael Michael, 20 na Edian Felician, 20.
|