09 May 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Mfanyabiashara Dar akatwa mapanga na kuporwa pesa
 
2008-05-09 19:18:56
Na Moshi Lusonzo, Muhimbili

Mfanyabiashara mmoja anayeishi Magomeni Moroco Jijini amelazwa katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili, MOI akiwa taabani baada ya watu wanaodaiwa kuwa vibaka kumkatakata kwa mapanga mwilini na kisha kumpora pesa zake kibao.

Mtu huyo aliyetambulika kwa jina la Ulomi Ngilay, 42, amepatwa na mkasa huo majira ya saa 1:30 usiku, eneo la bonde la Mkwajuni wakati akirudi nyumbani kwake.

Akisimulia kwa taabu akiwa wodini, Bw. Ulomi akasema siku ya tukio alikuwa akirejea nyumbani kwake akitokea kumjulia hali rafiki yake aliyekuwa akiishi mtaa wa jirani na ndipo alipokutwa na masahibu hayo.

Akasema wakati akirudi, njiani alikuwa akitembea na mzee mmoja, ambapo wote walipita katika bonde hilo huku kila mmoja akipita kivyake.

Akaeleza zaidi kuwa, kabla ya kumaliza bonde hilo, ghafla akastukia mtu mmoja akitokea kwa nyuma yake na kumkaba shingoni kwa nguvu. Baada ya kuona hali hiyo, anasema akaanza kujitetea kwa kujinasua katika kitanzi hicho.

``Nilijitahidi kujinasua hadi nikafanikiwa kutoka... hapo ndipo nilipoanza kujitetea kwa kupigana na mtu yule,`` akasema.

Hata hivyo, akiwa katika harakati hizo za kujiokoa, watu wengine watatu walitokea na kuanza kumkatakata mapanga mwilini na kusababisha kuishiwa nguvu.

Akasema, licha ya kipigo hicho, watu hao walifanikiwa kuondoka na pesa zake kiasi cha Sh. 200,000 alizokuwa nazo na simu yake ya mkononi.

Aidha, wanafunzi waliokuwa wakifanya mazoezi ya kukimbia, ndio waliomuokoa katika tukio hilo na kumsaidia kumfikisha katika Hospitali ya Mwanyamala kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Afisa Uhusiano wa MOI, Bw. Almas Jumaa akasema, mgonjwa huyo likafikishwa hapo majira ya saa 5:00 asubuhi akitokea Hospitali ya Mwananyamala baada ya kuonekana hali yake kuwa mbaya.

Baada ya kufanyiwa uchunguzi, ilibainika mguu wake mmoja ulivunjwa na moja ya mapanga hayo.

Hata hivyo, akasema hali yake kwa ujumla inaendelea vizuri baada ya kupatiwa matibabu.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.