|
Madenti wa shule za kijeshi Dar kufundishwa ukakamavu
2008-05-09 19:17:43
Na Abdul Mitumba, Temeke
Shule nne za sekondari zinazomilikiwa na Jeshi Jijini zimeanzisha utaratibu wa kutoa mazoezi ya ukakamavu kwa wanafunzi wake kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita.
Hatua hiyo imechukuliwa kwa nia ya kuwaweka wanafunzi katika hali ya ukakamavu ili uwasaide kujilinda, kulinda familia zao na taifa kwa ujumla.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Jitegemee, Meja Martine Mkisi, ameyasema hayo wakati akimkaribisha Luteni Kanali Dk. Amri Mwami kwa ajili ya kufunga mafunzo ya wiki tatu ya ukakamavu kwa wanafunzi zaidi ya 600 wa shule hiyo.
Amesema mafunzo hayo yametolewa na wataalam kutoka Jeshi la Wananchi na JKT kila siku mara baada ya vipindi vya masomo na kwamba zaidi ya wanafunzi 80 walifanya vizuri na kutunukiwa zawadi mbalimbali.
Meja Mkisi alizitaja shule nyingine zinazomilikiwa na Jeshi zinazoendesha mafunzo hayo Jijini kuwa ni Air Wing ya Ukonga, Navy ya Kigamboni na Makongo katika kambi yake ya Makongo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Luteni Kanali Dk. Mwami amesifu utaratibu huo, akisema kuwa siyo tu utawezesha wanafunzi kuwa walinzi wazuri wa miili yao na familia zao, lakini pia yatawaongezea ufahamu wakiwa darasani.
``Kwa ninavyofahamu, mtu mchangamfu ni rahisi kupokea mafundisho akiwa nje na ndani ya darasa... sasa naomba wakuu wa shule hizo za Jeshi watenge muda wa kuwasaidia wanafunzi katika shule za kawaida kuwapatia mafunzo hayo,`` amesema.
Ameongeza kuwa kila penye wanafunzi au watu wakakamavu huwa rahisi kwao kupambana na kila jambo linalotokea mbele yao ikiwemo kufikiri kwa haraka na kutoa uamuzi.
Dokta Mwami pia ameisifu sekondari ya Jitegemee kwa kufanikisha mafunzo hayo, akisema licha ya muda mfupi uliotumika, lakini amesema kuwaweka pamoja watoto ambao kila mmoja ametoka shule yake ni jambo kubwa na linalostahili pongezi.
|