07 May 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

DC K`ndoni ataka Mkurugenzi kutowakumbatia wabadhirifu
 
2008-05-07 19:41:50
Na Francisca Jeremiah, Kinondoni

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Kanali Mstaafu Fabian Massawe, amemtaka Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Bw. Noel Mahyenga, kuwadhibiti watendaji pamoja na madiwani wake ili wasiwe wabadhirifu wa fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya kuleta maendeleo ya wananchi wake.

Bw. Massawe ameyasema hayo wakati alipokuwa akizungumza na Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo, lililofanyika katika ukumbi wa Manispaa hiyo ambalo lilikuwa likipitisha bajeti ya mwaka 2008/09 ya mpango wa makadirio na mapato ya matumizi kwa kipindi kijacho.

Akasema Halmashauri imetenga Sh. billion 43 kwa bajeti yake ya mwaka huu, ambazo zitatumika katika kuleta maendeleo ya wananchi kwa kuboresha miundombinu ambayo mingi bado ni mibovu na kuwa kero kwa wakazi wa Wilaya hiyo.

``Nawaomba waheshimiwa ,adiwani na watendaji kutumia kikamilifu fedha hizi kwa malengo ambayo yameidhinishwa ili kuweza kufikia lengo zuri kwa jamii na kuweza kuwatoa katika kero wanazokabiliana nazo hivi sasa... hivi sasa tuna kazi ya kuwapa huduma wakazi wapatao Milioni 1.3, `` akasema.

Bw. Masawe alisema imewapasa watendaji hao kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni za misingi ya Utawala bora ili waweze kuwaridhisha wanachi wao na kuleta maendeleo yanayoonekana kwa kuweza kuondokana na lawama wanazotupiwa za ubadhirifu wa fedha kwa baadhi ya viongozi wa Halmashauri hiyo.

``Fedha tumepata na tusiishie kusema tu. Tuwe watendaji wa kazi kwa kila mmoja ahakikishe anajipanga vema kufanya kazi kwa kujituma kwa bidii na si kwa kulazimishwa wala kusubiria kulipwa posho kwa kila kazi atakayofanya,`` akasema Bw. Massawe.

Akaongeza kwa kuwataka watendaji hao kuongeza juhudi katika ukusanyaji wa vyanzo vyao vya mapato ambapo bado zoezi hilo haliridhishi ukilinganisha na raslimali zilizopo.

``Sijui watendaji mnafanya nini?Bado tupo chini kiutendaji na sijui tatizo ni nini? Tupo nyuma , tujitahidi sasa na tuamke usingizini tufanye kazi kwa kasi kubwa ndipo tutafanikiwa na kufikia malengo yaliyokusudiwa... tuache uvivu na wizi wa fedha kwani tutazidi kurudi nyuma badala ya kusonga mbele,``akasema.

Naye mbunge wa Jimbo hilo Bw. Idd Azzan, aliitaka Manispaa hiyo kuimarisha utendaji wao wa kazi, hasa pale wanapokarabati ujenzi wa barabara.

Akasema kwa sasa Manispaa iachane na ukarabati wa kiwango cha changarawe na barabara hizo zijengwe kwa kiwango cha lami, kwani ujenzi wa changarawe huchangia kuharibika kwa barabara hizo haraka pale mvua zinaponyesha.

``Sasa Halmashauri ijipange vizuri... tunatumia gharama kubwa kujenga barabara za changarawe na matokeo yake ni sifuri,`` akasema.

Hata hivyo, diwani wa kata ya Kibamba, Bw. Ignas Mwitura, ameliomba Baraza hilo baada ya kupitisha bajeti hiyo kutoa kipaumbele kwa ujenzi wa mabomba yatoayo maji safi ambapo kwa sasa, amesema ni tatizo kubwa mno katika kata nyingi zilizopo kwenye halmashauri hiyo.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.