06 May 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Soo la kichwa: Dogo azua mapya
 
2008-05-06 16:13:49
Na Mwandishi Wetu, Kisutu

Ramadhani Musa, 18, yule dogo anayedaiwa kukutwa na kichwa cha mtoto, jana alizidi kuwachanganya watu waliofurika kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutokana na vimbwanga vyake na vitu visivyo vya kawaida alivyokuwa akifanya.

Ramadhani pamoja na mama yake Khadija Seleman, 38, walitinga maeneo ya Kisutu mishale ya saa 3:30 asubuhi kwa difenda la polisi huku wakiwa chini ya ulinzi mkali wa askari wenye silaha.

Vimbwanga vilianza mahakamani hapo baada ya dogo huyo
kushushwa kutoka kwenye difenda.

Watu kibao waliofika kumwona `laivu` walijikuta wakiingiwa na hofu na kusogea mbali kabisa na alipokuwa anapitishwa.

Hata hivyo dogo huyo alikuwa akigeuka geuka kana kwamba nyuma kuna mtu mwingine anamsubiri.

Maafande kwa upande wao walikuwa wakihaha kutazama kila upande kuhakikisha kunakuwa na usalama mkubwa kwa dogo huyo.

Hali hiyo ilitokana na hisia kwamba wananchi wenye hasira wangeweza kumdhuru.

Mahabusu wengine ambao waliletwa mahakamani hapo kwa usafiri wa karandinga, hawakupata nafasi ya kumuona dogo huyo `laivu` kwani maafande walikuwa tayari wameweka utaratibu mzuri ili wakiingia tu, kijana huyo na mama yake nao wawe wameondolewa.

Hata baada ya kuingizwa ndani ya ukumbi wa kusikilizia kesi na mahakama kuanza shughuli zake, Ramadhan hakuonekana kujali kinachoendelea na badala yake muda mwingi akawa anaangalia darini utadhani kuna vitu alikuwa akifuatilia.

``Yaani utadhani kule darini kuna sinema anatazama. Muda wote anaangalia huko tu,`` mmoja wa watu waliofika mahakamani hapo aliliambia gazeti hili.

Hatua hiyo ilisababisha askari kumuonya mara kwa mara na kumtaka akae kwa heshma akitambua kuwa yuko mahakamani, sehemu ambayo ina kanuni na taratibu zake.

Wakati wa kusomewa shitaka ulipowadia, Hakimu alianza kuwaeleza watuhumiwa kuwa hawatakiwi kujibu lolote kwa vile mahakama hiyo haina uwezo wa kisheria kusikiliza kesi yao.

Hata hivyo baada ya Mwendesha Mashtaka, Kamishna Msaidizi wa Polisi Charles Kenyela kumaliza kuwasomea shitaka lao la mauaji, mama wa Ramadhani alijibu na kusababisha kurudiwa upya kusomwa shitaka hilo.

Kabla ya kusoma kwa mara ya pili, Kamishna Kenyela alimwomba Hakimu awaonye tena watuhumiwa wasijibu lolote.

Baada ya kumaliza kusomewa shitaka lao, watu wote waliokuwemo ndani ya mahakama walitakiwa kutoka nje ili kupisha watuhumiwa hao waondolewe.

Kamisha Kenyela aliiambia mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na hivyo ikaahirishwa hadi Mei 19, mwaka huu itakapotajwa tena mahakani hapo.

Ramadhani na mama yake, wakazi wa Tabata Segerea kwa Bibi wanatuhumiwa kumuua mtoto Salome Yohana, 3, mnamo Aprili 25 mwaka huu huko Segerea kwa Bibi wilaya ya Ilala, mkoani Dar es Salaam.

  • SOURCE: Alasiri
Tuma Maoni Yako
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.