|
Waandishi wa habari wapewa changamoto
2008-05-06 16:08:38
Na Adam Fungamwango, Jijini
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo wa Zanzibar, Mh. Mahmood Thabit Kombo, amewapa changamoto waandishi wa habari nchini kwa kuwataka wajiamini katika kazi zao ili kuongeza ufanisi.
Naibu Waziri huyo amesema waandishi hawapaswi kuwahofia watu kwa umaarufu wao au vyeo vyao na kushindwa kutekeleza vyema majukumu yao.
Akifungua maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, pale kwenye hoteli ya Peacock Jijini, Mh. Kombo akasema baadhi ya waandishi wa habari wamekuwa hawajiamini wanapokwenda kutafuta habari, hivyo kuwafanya wasipate yale wanayoyakusudia toka kwa chanzo na badala yake kugeuziwa kibao wao kwa kuulizwa maswali badala ya kupokea majibu.
Naibu Waziri huyo akasema sababu kubwa anayoiona ni mwandishi mwenyewe kuwa na uelewa mdogo wa kile ambacho anakwenda kukitafuta kwa mtoa habari, jambo ambalo humfanya akose maswali ya maana na mwishowe kuonekana wazi kuwa hajiamini.
``Kuna mwandishi mmoja alishawahi kunihoji... nilipomchunguza, nikabaini kuwa hana uelewa wa kutosha kuhusiana na kile alichokuwa akikitaka toka kwangu. Nami nikampa changamoto kwa kumgeuzia kibao na kuanza kumuuliza maswali yeye mwenyewe... ni vyema mkawa na uelewa wa jambo husika ili muweze kujiamini na kufanya kazi zenu kwa ufanisi zaidi,`` akasema Naibu Waziri huyo.
Mh. Kombo alisema kuwa waandishi wanatakiwa kabla ya kwenda kuhoji kile ambacho anatakiwa awe na uhakika na kile anachotaka kwenda kumhoji kiongozi, au mtu yoyote kwa kukifanyia utafiti, kukichunguza au kukisoma ili akimfikia awe anajua ni maswali gani ya kuuliza na si kwa kubahatisha.
``Unasoma kwanza, hivi inakwenda hivi na mimi nitaanzia hapa kumhoji, kwa hiyo hapo utamuuliza mtu kwa ufasaha na ile tabia ya kutojiamini itatoweka kwa sababu una uhakika na kile unachokihoji,`` akasema .
Maadhimisho hayo yaliandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari nchini, TAJA na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa tasnia ya habari.
|