|
Profesa Maghembe kuzindua mafunzo kwa wenye shule, vyuo
2008-05-06 16:07:21
Na Sabato Kasika, Jijini
Waziri wa Elimu Prof. Jumanne Maghembe anatarajia kuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa semina ya kuwajengea uwezo wamiliki binafsi wa shule na vyuo nchini.
Akizungumza na Alasiri Jijini, Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Shule na vyuo binafsi, Bw. Benjamin Nkonya, amesema semina hiyo itafanyika kesho na kwamba baadhi ya mada zitakazojadiliwa ni pamoja na sheria mbalimbali kuhusiana na utoaji wa elimu.
Bw. Nkonya akaongeza kuwa mada nyingine zitakuwa ni kuhusu sheria ya uendeshaji wa shule, sheria ya kodi, uwekezaji, mikopo na mifuko ya hifadhi ya jamii.
Akasema kwamba watoa mada watatoka katika maeneo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na idara za serikali, mashirika na wakufunzi binafsi.
``Tunataka kuwajengea uwezo wamiliki binafsi wa shule na vyuo ili wawe na uelewa mpana wa sekta ya elimu nchini kabla na baada ya shule zao kupata usajili,`` akasema Bw. Nkonya.
Akasema chama chao kimeandaa semina kama hizo katika kanda zote nchini.
Akasema mkoa wa kwanza kupata mafunzo hayo ni Dar es Salaam, kisha itafuatia mikoa ya Pwani, Morogoro, Dodoma, Lindi na Mtwara.
Akasema baada ya hapo itakuwa ni zamu ya mikoa ya Kanda ya Kaskazini ya Arusha, Manyara, Kilimajnaro na Tanga.
Katibu huyo akasema kuwa baadaye watafanya semina kama hizo katika mikoa ya Kanda ya Ziwa inayojumisha Kagera, Mwanza, Mara na Shinyanga, kisha watakwenda Singida na kumalizia Mbeya, Iringa, Rukwa na Ruvuma.
|