|
Manispaa K`ndoni kukarabati mitaro yote ya maji machafu
2008-05-06 16:06:19
Na Valery Kiyungu, Kinondoni
Mwenyekiti wa Mipango Miji katika Manispaa ya Kinondoni, Bw. Rajabu Hassan, amesema ofisi yao iko katika mchakato wa kukarabati mitaro yote ya kupitisha maji machafu iliyoko katika Manispaa yao ili kuimarisha hali ya usafi na pia kurahisisha utunzaji wa barabara.
Na kwa kuanzia, Bw. Hassan amesema watafanya zoezi hilo kwenye kata saba ikiwemo ya Manzese ambayo karibu mitaro yake yote imeziba, kisha wataendelea katika kata nyinginezo.
Bw. Hassan amesema hayo katika mahojiano maalum kuhusiana na mikakati ya ofisi yake, ambapo pamoja na mambo mengine, amesema katika bajeti ijayo ya mwaka huu, wamepanga kukarabati mitaro yote na hivyo kukamilisha zoezi hilo.
Amesema maazimio hayo yamefikiwa katika kikao cha hivi karibuni cha wajumbe wa kamati yao ya mipango miji, ambapo pamoja na mambo mengine, kwa kauli moja wamekubali kuwa baada ya kutengewa bajeti ya fedha, wafanye zoezi hilo la kusafisha mitaro ya maji machafu.
Amesema imebainika kuwa mitaro iliyoko katika hizo saba ipewe kipaumbele katika ukarabati huo kutokana na ukweli kuwa mifereji iliyoko kwenye kata hizo iko katika hali mbaya zaidi na hivyo kusababisha nyumba za wakazi kufurika maji pale panaponyesha mvua, hata kama mvua zenyewe si kubwa sana.
Ukiondoa Manzese, kata nyingine zitakazonufaika na zoezi hilo ni za Mwananyamala, Ndugumbi, Tandale, Hananasif, Magomeni na Mzimuni.
``Maandalizi kwa ajili ya zoezi hilo yameanza na tunaamini kuwa kila kitu kitakwenda kama kilivyopangwa,`` akasema Bw. Hassan.
Bw. Hassan amesema hatua hiyo ya ofisi yake kuanza ukarabati kwenye kata hizo, inalenga katika kuwaondolea kero ya muda mrefu wakazi wa maeneo hayo ambao baadhi nyumba zao hujaa maji wakati wa mvua.
Wakati huo huo Bwana Rajabu amesema kuwa uongozi wake baada ya kukamilisha zoezi zima la kukarabati mitaro, umepanga kupambana na watu ambao wana tabia ya kutupa taka kwenye mitaro ya maji machafu.
Akasema hatua mojawapo ni kuwaburuza kortini watu wote watakaoendelea kutupa taka kwenye mitaro ya kupitishia maji machafu na yale ya mvua.
|