|
Sakata la kichwa cha mtoto: Watuhumiwa kortini
2008-05-05 18:30:44
Na Mwandishi Wetu, Kisutu
Ramadhani Musa, yule dogo aliyedaiwa kukutwa akila kichwa cha mtoto Jumapili iliyopita na sakata hilo kuzua hofu kubwa nchini, leo amefikishwa mahakamani, yeye na mama yake mzazi, Hadija Selemani.
Wawili hao walifikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi Kisutu mishale ya saa 3:30 asubuhi wakiwa ndani ya difenda huku wakisindikizwa na askari kibao, baadhi wakiwa na mitutu na wengine wamevalia kiraia.
Katika hali ya kushangaza, watu waliokuwa kortini walijikuta wakisogea mbali kabisa na mtuhumiwa huyo, totauti na siku zote anapofikishwa mahakamani mtu ambaye kesi yake imegusa hisia za watu wengi.
Walioshuhudia watuhumiwa hao wakitinga kortini, wanasema, waliothubutu kusogea karibu na dogo huyo ni wapiga picha na mapaparazi tu.
Hati ya mashitaka ya kesi hiyo inaonyesha kuwa, watuhumiwa Ramadhani na Hadija, wote wakazi wa Segerea kwa Bibi, usiku wa Aprili 25 mwaka huu, huko Segerea kwa Bibi, walimuua mtoto Salome Yohana.
Hadi gazeti hili linakwenda mitamboni, kesi hiyo ilikuwa bado haijapangiwa hakimu na watuhumiwa walikuwa bado rumande ya mahakama hiyo.
|