05 May 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Apigwa na kuporwa pesa, simu
 
2008-05-05 18:28:17
Na Moshi Lusonzo, Muhimbili

Mkazi mmoja wa Ubungo Urafiki Jijini, amelazwa katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili, MOI huku akiwa katika hali mbaya baada ya kupata kipigo kutoka kwa watu wanaodaiwa kuwa ni vibaka.

Mtu huyo aliyetambulika kwa jina la Elias Lyakwika, 23, alipatwa na tukio hilo juzi majira ya saa 12:00 alfajiri wakati akiwa karibu na daraja jipya la Ubungo.

Akizungumza kwa taabu, Lyakwika amesema kuwa siku alipopatwa na tukio hilo alikuwa akirejea nyumbani baada ya kufanya kazi ya kusafirisha watu usiku kwa kutumia gari lao.

Akasema, baada ya safari yao ya mwisho waliyoifanya kati ya Ubungo na Vingunguti, wakaamua kurudisha gari sehemu inapolala na wao wakaanza kutembea kwa miguu kuelekea majumbani mwao.

Lakini, anasema alipofika eneo la daraja, ghafla likaibuka kundi la watu na kuanza kumpiga huku wakimuamuru kutoa kila kitu alichokuwa nacho.

Akasema watu hao walifanikiwa kuchukua simu moja na shilingi 12,000 ambazo alikuwa amezipata siku hiyo.

``Walinipiga kwa kutumia silaha mbalimbali ikiwa ni pamoja na machepe ya kuzolea mchanga ... nikaumia sana kama unavyoniona,`` akasema Lyakwika.

Katika tukio hilo, Lyakwika akaumia vibaya kichwani na mabegani kwa kukatwakatwa na chepe na kumfanya awe na majeraha makubwa katika sehemu hizo.

Afisa Uhusiano wa MOI, Bw. Almas Jumaa, amesema mgonjwa huyo alifikishwa hapo majira ya saa 2:00 asubuhi akitokea katika Hospitali ya Mwananyamala baada ya hali yake kuwa mbaya.

Akasema, alifikishwa hapo akiwa katika hali mbaya na haraka alikimbizwa wodi namba 17 jengo la Sewahaji kwa ajili ya kupatiwa huduma za matibabu.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.