02 May 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Mtoto mla vichwa: Wazazi BP juu!
 
2008-05-02 18:14:07
Na Emmanuel Lengwa, Jijini

Matukio ya mauaji na utekaji wa watoto yanayoambatana na imani za ushirikina yaliyozua gumzo Jijini yameanza kuwapa presha `BP` baadhi ya wazazi ambao sasa wamedai kuhofia maisha ya watoto wao.

Wakizungumza na Alasiri, baadhi ya wazazi hao wamesema wamesema matukio ya kishirikina yaliyolitikisa Jiji wiki hii, hasa lile la mtoto wa miaka mitatu kuchinjwa na kichwa chake kukutwa kikifyonzwa damu na mtoto mwingine, yamewasababishia hofu kubwa katika kipindi hiki ambacho watoto wao wangali wakienda shule.

``Niseme ukweli kuwa baadhi ya wazazi tumeingiwa na hofu... hawa washirikina wanatufanya tuamini kuwa watoto wetu pia wanawindwa. Ni vyema kila mmoja akawa tayari kuwapa taarifa polisi ili watu wa namna hiyo wakamatwe,`` akasema akasema Bi. Mwanaisha Ally, mkazi wa Tandale.

Mkazi mwingine aliyedai kuwa ni wa Tabata Relini, Bw. Josephat Hamza amesema licha ya Serikali kutoamini ushirikina, lakini inapaswa kuangalia uwezekano wa kukomesha vitendo kama hivyo ambavyo vimekuwa vikiwapotezea maisha watu wasio na hatia.

``Ingawa Serikali haiamini ushirikina, lakini tunaamini bado inayo nafasi ya kulishugulikia suala hili kwa kina na kukomesha kabisa vitendo hivyo. Kama watashirikiana na viongozi wa dini katika kuwaelimisha watu juu ya madhara ya imani potofu za kishirikina, ni wazi kwamba roho za watu wasio na hatia zitaweza kusalimika,`` akasema.

Mwingine aliyejitaja kwa jina moja la Prisca, mkazi wa Manzese Jijini, amesema hivi sasa amekuwa akiingiwa na hofu kila mara anapoona mwanawe wa miaka saba akichelewa kurejea nyumbani toka shuleni.

``Ni tukio lililotokea Tabata... lakini wapo watoto wengine waliopotea na taarifa zao hazijajulikana. Kwa sababu hiyo, huenda wauaji hawa wako maeneo mengi zaidi na ndio maana nimekuwa na hofu kila mara mwanangu anapochelewa kurudi,`` akasema Bi. Prisca.

Katika tukio lililoshtua wengi na kuwafanya baadhi ya wazazi kuwa roho juu, mtoto Ramadhan Musa, 12, alikamatwa Jumamosi iliyopita katika maeneo ya Muhimbili akiwa na kichwa cha mtoto aliyetambuliwa baadaye kuwa ni Salome Yohana, 3.

Mtoto Ramadhani alikutwa akikinyonya damu kichwa hicho cha mtoto Salome, ambaye alitoweka kwao na kisha kiwiliwili chake kuokotwa kwingine, huku kikiwa bila kichwa.

Hadi sasa, mtoto Ramadhani anashikiliwa na Polisi ambao bado wanaendelea na uchunguzi mkali kuhusiana na mkasa huo wa kuogofya.

Tukio la pili ni lile lililotokea juzi ambapo mtoto Margaret Kefa, 16, ameripotiwa kukamatwa katika wodi ya wazazi ya Kituo cha Afya Tabata Segerea.

Mtoto huyo alipohojiwa, alisema ametumwa na bibi yake kuwaua watoto wachanga na kuchukua damu yao ili ampelekee akainywe.

Asubuhi ya leo, Alasiri lilifanya jitihada za kumsaka Kamishna wa Kanda Maalum ya ya Polisi Jijini Dar, Alfred Tibaigana, ili kuzungumzia hali hiyo ya hofu kwa baadhi ya wazazi katika eneo lake.

Hata hivyo, Kamanda Tibaigana hakuweza kupatikana baada ya kuwa mkutanoni, kwa mujibu wa maelezo ya wasaidizi wake.

Aidha, Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Ilala Faustine Shilogile, ambaye ndiye mwenye eneo la Tabata lililoripotiwa matukio hayo, pia hakuweza kupatikana.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.