|
SUMATRA yakoromea upandishaji nauli kiholela
2008-05-02 18:02:05
Na Job Ndomba, Jijini
Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi kavu na Majini `SUMATRA` imepiga marufuku upandishwaji wa nauli kiholela unaofanywa na daladala na mabasi yaendayo mikoni kwa kisingizio cha mafuta.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa SUMATRA kwenda kwa vyombo vya habari, imeelezwa kuwa upandishwaji wa nauli kiholela unaoendelea hivi sasa, upo nje ya taratibu zilizokubaliwa kisheria.
Taarifa hiyo imesema kuwa kufanya hivyo ni kuvunja sheria.
Mamlaka hiyo imesisitiza kuwa taratibu za kupandisha nauli hufanyika kwa kuwasilisha maombi rasmi na kuhauriana na wadau na kufanyia uchambuzi mapendekezo yanayowasilishwa kwa kutumia vigezo maalum.
Imesema kuwa vigezo vinavyoangaliwa na kufanyiwa upembuzi ni pamoja na kupanda kwa bei ya mafuta, gharama za uendeshaji na mfumuko wa bei kwa ujumla kwa mujibu wa vifungu vya sheria ya SUMATRA.
Aidha, imewataka wamiliki na madereva wa mabasi kutoa ushirikiano na kuhakikisha kuwa viwango vya sasa vinazingatiwa.
Sambamba na hilo SUMATRA imewataka abiria kutoa taarifa kuhusu upandishwaji wa nauli kiholela ili mamlaka iweze kuchukua hatua zinazostahili.
Hivi karibuni, baadhi ya wamiliki na magari ya kusafirisha abiria yakiwemo mabasi yaendayo mikoani na daladala wamejiamulia kupandisha nauli kwa maelezo kuwa bei ya mafuta imepanda mno na hivyo kuongeza gharama za uendeshaji.
|