02 May 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Zimamoto kutoa elimu kuhusu sheria mpya ya kudhibiti moto
 
2008-05-02 18:00:33
Na Francisca Jeremiah, Jijini

Kikosi cha Zimamoto nchini ambacho kipo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi, kinatarajia kuitangaza sheria mpya ya moto na uokoaji, itakayoshirikisha utendaji wa kazi kati ya jamii na Serikali na kutoa mwongozo wa namna ya kujikinga na majanga ya moto na maafa.

Sheria hiyo inatarajiwa kutangazwa mwanzoni mwa mwezi Mei na kuanza kufanya kazi baada ya kutangazwa kwake.

Hayo yamesemwa na Kamishna Mkuu wa Kikosi cha Zimamoto nchini, Bw. Sotery Ntamuturano, wakati alipokuwa akizungumza na Alasiri ofisini kwake Jijini Dar es Salaam, juu ya muundo huo mpya wa sheria hiyo.

Alisema sheria hiyo imeshasainiwa na Mhe. Rais Jakaya Kikwete tangu mwaka jana na kilichobaki ni kutangazwa na Waziri wa Wizara hiyo Bw. Lawrence Masha ili ianze kutumika.

Bw. Ntamuturano amesema kuwa sheria hiyo imeundwa kwa lengo la kuishirikisha jamii katika kujikinga na majanga ya moto na maafa, ambayo yamekuwa yakitokea kila mara nchini na kusababisha hasara kubwa.

``Matatizo ya kutokea kwa majanga ya moto yamekuwa yakikithiri nchini... Serikali imeamua kufanya maamuzi mbalimbali ya kupunguza tatizo hilo ikiwa ni pamoja na kununua magari zaidi ya zimamoto, kutoa mafunzo mbalimbali kwa jamii na pia kusisitiza juu ya hulka ya kuchukua tahadhari ya kujilinda na majanga hayo,`` akasema Kamishna huyo.

Akasema vyanzo vingi vya moto hutokea katika umeme wa majumbani, hasa matumizi mabaya ya vitu vya umeme kama majiko.

Aidha, akasema sababu nyingine za kuzuka kwa majanga ya moto ni kukatika hovyo kwa umeme na milipuko ya transfoma za umeme.

Hata hivyo, akasema Kikosi cha Zimamoto kimekuwa kikijitahidi kushirikiana na wananchi katika kupambana na majanga hayo na yale ya utupwaji wa watoto vyooni.

  • SOURCE: Alasiri
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.