|
Kandoro aagiza shule zote za sekondari zijengwe kwa wakati
2008-05-02 17:55:58
Na Haji Mbaruku, Jijini
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam ameziagiza Halmashauri za Jiji lake kuhakikisha kuwa ujenzi wa shule za Sekondari unakamilika kwa wakati.
Bw. Kandoro ambaye ndiye aliyeanzisha mchakato wa kuchangisha fedha kwa ajili ya ukarabati wa shule hizo, amesema kuwa ni vyema ujenzi huo ukakamilika haraka ili wanafunzi waanze kusoma.
Alikuwa akiongea na kituo kimoja cha redio jijini kuhusiana na ujenzi wa shule za sekondari unaoendelea jijini.
Amesema kuwa, halmashauri za jiji za mkoa wa Dar es salaam hazina budi kuhakikisha kuwa ujenzi huo unakamilika haraka ili shule hizo zianze kutumika mara moja.
Amesema kuwa, mkoa wa Dar es salaam unataka kuhakikisha kuwa hakuna mwanafunzi aliyefaulu kuingia kidato cha kwanza, anakosa nafasi.
Bw.Kandoro amesema hayo kufuatia mikoa mingi kushindwa kuchukua wanafunzi wengi waliofaulu na kusababisha wakose haki ya kupata elimu.
Ndio maana alianzisha mkakati kabambe wa kuchangisha kwa ajili ya kujenga shule za sekondari za kata ambazo zitahakakikisha zinachukua wanafunzi wote wanaofaulu kujiunga na kidato cha kwanza.
Wazazi, mashirika na makampuni mengi yalijitokeza kuchangia ujenzi wa shule za sekondari mkoa wa Dar es salaam ambapo zaidi ya shilingi milioni 800 zilipatikana.
|