|
Wenye mabanda ya biashara Soko la Nyuki Tegeta waonywa
2008-04-30 18:29:55
Na Valery Kiyungu, Tegeta
Wamiliki wa vibanda vya maduka ambao wamejenga kwenye eneo la soko la Nyuki-Tegeta lililoko nje kidogo ya Jiji la Dar, wamepewa muda wa mwezi mmoja kuanza kuvitumia vibanda hivyo, vinginevyo nafasi zao watapewa watu wengine ili waendeshe shughuli za biashara.
Akizungumza na Alasiri ofisini kwake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Wafanyabiashara Soko la Nyuki-Tegeta (UWASOTE), Bw. Weche Moshi, amesema baadhi ya wafanyabiashara wamevitelekeza vibanda vya maduka kwenye eneo la soko baada ya ujenzi wake kukamilika.
Bw. Moshi amesema baadhi ya wafanyabiashara, awali walituma maombi katika ofisi za soko la Nyuki kutaka wapatiwe nafasi za kujenga vibanda vya biashara, ambapo hata hivyo, baada ya kukamilisha shughuli za ujenzi, wamevitelekeza vibanda hivyo na kuingia mitini na hivyo amewataka waanze biashara haraka kabla hawajanyang`anywa fursa hiyo na kupewa wengine.
``Wafanyabiashara ambao wametelekeza vibanda vyao vya biashara kwenye eneo la soko la Nyuki tumewapa mwezi mmoja kuanzia sasa wawe wameshaanza biashara... ikifika Mei 15 na bado wakawa wamevifunga vibanda hivyo bila kuvifanyia kazi, tutachukua hatua ambazo bila shaka zitawaengua wababaishaji na kuwapisha waliopania kweli kufanya biashara,`` akasema.
Moshi amesema mara kadhaa ofisi yake imekuwa ikipokea maombi toka kwa wafanyabiashara wakitaka wapatiwe nafasi hizo, hivyo uongozi wake umeona ni vyema kuwapa nafasi wale waliowahi kuanza biashara kwani vinginevyo, hawatakuwa na jinsi isipokuwa kutoa nafasi hizo kwa wengine wenye nia ya kweli ya kufanya biashara.
|