|
Soo la Richmond:Haponi mtu!
2008-03-18 15:30:04
Na Emmanuel Lengwa, Jijini
Kitimtim cha aina yake, kama kile kilichozuka mwezi uliopita baada ya kuwasilishwa kwa ripoti ya Kamati Teule iliyoundwa na Bunge kuchunguza sakata la mkataba tata wa Richmond, kinatarajia kutimka upyaa baada ya tume ya Waziri Mkuu kukabidhi ripoti yake.
Habari zilizolifikia gazeti hili zinadai kuwa tume hiyo iliyoundwa na Waziri Mkuu Bwana Mizengo Pinda kupitia mapendekezo yaliyotolewa na Kamati Teule iliyoundwa na Bunge kuchunguza mkataba tata wa Richmond, imemaliza kazi yake na kutoa mapendekezo kadhaa ambayo huenda yakawamwaga vigogo kibao bila huruma.
Taarifa zaidi zinadai kuwa tume hiyo ya Bw. Pinda, imeridhia mapendekezo kadhaa yaliyotolewa na kamati teule ya Bunge iliyokuwa ikiongozwa na Mbunge wa Kyela,
Dk. Harrison Mwakyembe.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, tume hiyo imefanya kazi hiyo kwa uadilifu mkubwa bila hofu wala upendeleo.
Inasemekana kama ilivyokuwa kwa kamati ya akina Mwakyembe, tume hiyo pia imefanya ufuatiliaji wake na kutoa ushauri na mapendekezo kadhaa.
Tayari Waziri Mkuu, Bw. Pinda amethibitisha kuwa ripoti ya tume hiyo iko tayari na anatarajia kuipokea wiki hii kutoka kwa Katibu Mkuu.
Waziri Mkuu Pinda amesema mara baada ya kuipokea taarifa hiyo, atakaa na baadhi ya mawaziri kujadili mapendekezo hayo kabla ya kumshauri Rais Jakaya Kikwete hatua za kuchukua.
Ripoti ya Kamati Teule ya Bunge iliyowasilishwa Bungeni na Mwenyekiti wake Dk. Mwakyembe, ilikuwa na mapendekezo 16 ikiwemo kuwawajibisha baadhi ya vigogo waliohusishwa kwa njia moja ama nyingine na sakata la Richmond.
Kamati hiyo ilipendekeza vigogo kadhaa wawajibishwe. Baadhi yao ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Bw. Edward Hosea, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw. Johnson Mwanyika, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini pamoja na vigogo wengine waliohusishwa katika sakata hilo.
Baadaye Waziri Mkuu mpya Bw. Pinda aliunda tume ya kufuatilia mapendekezo hayo ambayo sasa imekabidhi ripoti yake.
|