|
Duka la nguo za maharusi Dar lawaka
2008-03-18 15:25:46
Na Haruni Sanchawa , Jijini
Moto mkali umeteketeza duka moja la nguo za maharusi na nyinginezo za aina mbalimbali Jijini na kusabaisha hasara inayokadiriwa kuwa ya mamilioni ya pesa.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Ilala, Faustine Shilogire, amelitaja duka hilo kuwa ni Tausi Fashion Enterprises Ltd lililokuwa katika Jengo la SIDO, barabara Bibi Titi Mohamed.
Kamanda Shilogire amesema uchunguzi kuhusiana na chanzo cha tukio hilo bado unaendelea.
Hata hivyo, akasema kuwa uchunguzi wa awali kuhusiana na tukio hilo, unaonyesha kuwa chanzo ni hitilafu ya umeme iliyotokea katika ofisi jirani ya duka hilo.
Akasema kufuatia ajali hiyo, kila kilichokuwamo ndani ya duka hilo kimeungua na hivyo kusababisha hasara kubwa.
``Sisi tulipata taarifa baadaye kwa njia ya simu toka kwa mtu mmoja aliyetueleza kuwa ndiye mmiliki wa duka... alituambia kuwa duka lake lenye kujihusisha na uuzaji wa nguo za aina mbalimba za maharusi pale katika barabara ya Bibi Titi Mohamed linateketea kwa moto,`` akasema Kamanda Shilogire.
Akasema polisi walifika eneo la tukio na kushuhudia askari wa kikosi cha zimamoto wakijitahidi kuuzima moto huo, lakini haikuwezekana kuokoa chochote isipokuwa kuuzima ili usisambae zaidi na kusababisha madhara katika maeneo mengine.
Aidha, akizungumza na Alasiri jana katika yake ofisi yake nyingine, Mkurugenzi wa kampuni hiyo Bi. Tausi Moshi, amesema hasara aliyoipata kutokana na moto huo inakadiriwa kuwa zaidi ya shilingi milioni 50, ambayo imetokana na samani zilizokuwamo na nguo za aina mbalimbali zikiwemo za maharusi kutoka Marekani.
``Nilipata taarifa nikiwa nyumbani kuwa ofisi yote imeungua... baada ya kufika kwenye eneo hilo, kweli nikakuta majivu tu... inasikitisha sana,`` akasema Bi. Tausi.
|