|
Upatikanaji umeme wapunguza matukio ya moto Jijini
2008-02-28 17:41:31
Na Francisca Jeremiah, Jijini
Kupungua kwa mgao wa umeme mwaka uliopita kumesaidia kupunguza matukio ya moto Jijini kulinganisha na mwaka 2006.
Akizungumza na Alasiri hivi karibuni, Mkuu wa Kikosi cha Zimamoto Jijini, Bw. Fikiri Salla, amesema tatizo la mgao wa umeme Jijini ndilo lililochangia kuwepo kwa matukio mengi ya moto mwaka 2006 huku kupungua kwake.
Akasema jambo hilo linatokana na ukweli kuwa matukio hayo, mengi huwa ni ya kuungua kwa ofisi na nyumba, sababu hasa ikiwa ni utumiaji holela wa mishumaa na jenereta.
Akasema mwaka 2006 kulikuwa na matukio 455, wakati mwaka jana kulikuwa na matukio 416.
``Ni vyema wananchi wakachukua tahadhari zaidi za kukabiliana na majanga ya moto.... kinyume chake, kama inavyofahamika, madhara huwa makubwa na yenye kusikitisha,`` akasema.
Akataja baadhi ya tahadhari hizo kuwa ni kufunga vifaa maalum vya moto katika ofisi na majumba.
``Pia kuwa na visima vya maji kwa wale wenye majengo marefu ili kurahisisha zoezi la uzimaji wakati majanga ya moto yanapotokea,`` akasema.
Katika hatua nyingine, Bw. Salla amesema ili kupambana vyema na majanga ya moto na uokoaji Jijini, kikosi chake kinahitaji kuongeza vituo vingine kwa kila wilaya.
Bw. Salla akasema kurahisisha utendaji wa kazi na kukabiliana na majanga ya moto, kikosi chake kinahitaji kila wilaya kuwe na vituo viwili vya zimamoto na askari wa kutosha.
``Majanga ya moto ni mengi na Jiji hili limepanuka kwa kiasi kikubwa... hivyo kinachohitajika ni kuongeza vituo vingine ili tuweze kupambana na tatizo hilo ambalo hutokea kila mara,``akasema Bw. Salla
Akasema hivi sasa, Jiji lina vituo pekee vya Zimamoto, ambavyo bado havitoshelezi mahitaji kutokana na ukubwa wa eneo.
|