|
Mihela ya BoT moto
2008-02-28 17:40:13
Na Emmanuel Lengwa, Jijini
Lile sakata la ufujaji wa mabilioni ya pesa za umma katika Benki Kuu, BOT limechukua sura mpya baada ya walaji wote kujikuta wakikabiliana na kibano kikali huku mapesa yenyewe yakiwa kama jinga la moto.
Waliokomba mapesa hayo kiasi cha Sh. Bilioni 133 za akaunti ya madeni ya nje, EPA, sasa wamejikuta wakiwa katika hali mbaya zaidi baada ya majina yao kutambulika, mali zao na mahala walikozichimbia pia kujulikana.
Imeelezwa kuwa watu hao wamekuwa wakibanwa mbavu kila kukicha kiasi cha kuwafanya wengi wao kuanza kuzirudisha, taka wasitake.
``Wengi hivi sasa wanajuta... kibano wanachokipata katika ufuatiliaji kimewaogopesha mno,`` amesema afisa mmoja wa Serikali aliyekataa kujitaja jina.
Aidha, taarifa iliyotolewa na timu nzito ya uchunguzi iliyoundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bwana Jakaya Kikwete, inasema hadi sasa, watafunaji kadhaa wameshajisalimisha na kurejesha mapesa hayo.
Timu hiyo iliyoundwa na Rais, imesema katika taarifa yake kuwa kazi inaendelea vizuri na hivi sasa, tayari imeshawatambua karibu wahusika wote waliolamba mapesa hayo.
Taarifa ya timu hiyo iliyotolewa kwenye vyombo vya habari, inaeleza kuwa hata mali nyingi za wahusika zimetambuliwa na kufahamika mahali zilipo.
``...mali zao nyingi zimetambuliwa na kufahamika, iwe zile zilizopo nchini na hata zilizopo nje ya nchi,`` ikasema sehemu za taarifa hiyo njema kwa Watanzania.
Aidha, taarifa hiyo imeelezea kuanza kurejeshwa kwa mapesa yaliyoliwa na hivyo kuleta matumaini kuwa mapesa yote yatapatikana.
``Fedha zilizolipwa isivyo halali zimeanza kurejeshwa Serikalini,`` imesema taarifa hiyo.
Timu hiyo imesema imejipanga vizuri kuhakikisha fedha zote zilizolipwa kinyume cha sheria kutoka kwenye akaunti ya malipo ya nje, EPA, zinarejeshwa.
Imeeleza zaidi katika taarifa yake kuwa hadi sasa, inaendelea kufuatilia kwa umakini taarifa zote zinazotolewa na wananchi kuhusu ufisadi huo.
Timu imewaomba wananchi wanaoelewa chochote kuhusiana na sakata hilo, waendelee kutoa taarifa moja kwa moja, kwa kupitia namba maalum ilizotoa ambazo ni 0713 223 362, 0784 213 928 na 0784 785 722.
Miongoni mwa wanaounda timu hiyo iliyotokana na ubadhirifu ulioainishwa na Mkaguzi aliyekodioshwa na Serikali, Ernst & Young ni Kamanda wa Jeshi la Polisi nchini, Said Mwema, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw. Johnson Mwanyika, Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, PCCB.
|