|
Mwanamke Dar adondoka ghorofani
2008-02-28 17:38:22
Na Kiyao Hoza, Polisi Kati
Mwanamke mmoja Jijini amejikuta akilazwa Muhimbili akiwa hoi baada ya kudondoka toka ghorofani huku mkazi mwingine wa Jiji aliyekuwa akiendesha baiskeli kufariki dunia baada ya kugongwa na gari.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Ilala, Masindoki Masindoki, amesema tukio la kwanza lililomuacha mwanamama mmoja akiwa hoi kwa majeraha limetokea jana, mishale ya saa 12:30 jioni katika maeneo ya barabara ya Uhuru.
Amesema mwanamama huyo, mfanyakazi wa kampuni ya usafi ya Semu, Bi. Maimuna Mohammed, 34, akiwa anafanya usafi katika njia ya lifti, katika jengo la Akiba, alidondoka toka ghorofa ya tatu hadi chini na kujeruhiwa vibaya katika sehemu mbalimbali za mwili.
Amesema majeruhi amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili akipatiwa matibabu na hali yake inaendelea vizuri.
Katika tukio jingine, mwendesha baiskeli, Mzee Mosha, 65, amefariki papo hapo baada ya kugongwa na gari wakati akikatiza barabara katika eneo la Bunale huko Chanika.
Kamanda Masindoki amesema tukio hilo limetokea jana mishale ya saa 9:00 alasiri, baada ya gari namba T 828 APK aina ya Escudo, kumgonga mwendesha baiskeli huyo.
Amesema gari hiyo ilikuwa ikiendeshwa na Deus Sillo, 23, wakati akitokea Pugu kuelekea Chanika.
Amesema maiti imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Amana na dereva anashikiliwa na polisi.
|